Kampuni ya jasi kuwekeza bil. 30/-

KAMPUNI ya utengenezaji wa jasi (gypsum) kutoka Ujerumani, KNAUF, imeingia rasmi katika biashara hiyo eneo la Afrika Mashariki na kuweka makao yake makuu nchini Tanzania, huku ikidhamiria kuwekeza kiasi cha dola milioni 15 (Sh bilioni 30) katika kipindi cha miaka michache ijayo, imefahamika.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa KNAUF Afrika Mashariki, Zachopoulos Georgios, hadi sasa wameshawekeza kiasi cha dola milioni 10 (shilingi bilioni 21) na ni matarajio yao kwamba watafikisha bilioni 30 katika kipindi cha muda mfupi ujao.

Kampuni hiyo ilianza rasmi shughuli zake nchini takribani miaka mitatu iliyopita na tayari imeajiri wafanyakazi 150; huku asilimia 99 kati yao wakiwa ni Watanzania. “KNAUF kwa sasa inafanya kazi katika nchi zaidi ya 200 hapa duniani lakini ofisi yake ya Tanzania ni ya kwanza miongoni mwa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Tumefanya makao yetu makuu kuwa Tanzania kwa sababu imekaa katika eneo la kimkakati kijiografia na inaweza kuwa mlango wetu wa kuingia katika nchi zisizo na bahari zinazoizunguka na mbali zaidi.

“Sababu nyingine iliyotufanya tuichague Tanzania ni ukweli kwamba kuna hali ya amani na utulivu,” alisema Mkurugenzi huyo aliyeongoza pia kwamba jasi wanayotumia inapatikana kusini mwa Tanzania Kampuni hiyo ya kimataifa pia ina mradi maalumu wa kufundisha vijana kuhusu teknolojia mpya za ufungaji na utengenezaji wa jasi; lengo likiwa ni kutoa mchango wao kwa jamii ya Tanzania.

“Mara wanapokuwa wamehitimu mafunzo yao, tunatoa vyeti ambavyo vinatambulika dunia nzima katika sekta ya ujenzi. Lengo letu ni kwamba hawa wanaofundishwa hapa waweze kuajiriwa popote duniani kwa sababu mafunzo yetu yana hadhi ya kimataifa,” alisema Georgios.

KNAUF Tanzania ni kampuni tanzu ya KNAUF yenye makao makuu yake nchini Ujerumani –ikiwa na maeneo ya uzalishaji na ofisi za mauzo 150 katika nchi zaidi ya 60 na ikiwa imeajiri wafanyakazi wa moja kwa moja 26,000 duniani kote.