Udadisi wa kaya awamu ya pili kuanza Agosti

IMEELEZWA kuwa Utafi ti wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania, Awamu ya Pili utafanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya wadadisi yanayoendelea kufanyika mkoani hapa jana, Meneja wa Shughuli za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Wilfred Mwingira alisema lengo kuu la utafiti huo ni kufuatilia viashiria vilivyowekwa kwenye utafiti wa Awamu ya Kwanza ili kutathmini na kujua kama kuna athari yoyote iliyotokea.

“Utafiti huu ni wa kitaifa na utafanyika Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kutathmini na kujua kama kuna athari yoyote iliyojitokeza kwenye viashiria vilivyowekwa kwenye utafiti wa awamu ya kwanza,” alisema Mwingira.

Naye Mratibu wa utafiti huo, Rainer Kiama amesema kuwa utafiti huu unafanyika ili kutathmini kama mpango unaleta manufaa yaliyokusudiwa katika ngazi ya kaya kwa kutumia viashiria kama vile elimu, afya, kazi na matumizi ya muda, shughuli za kaya zisizo za kilimo, mapato, mikopo, akiba na uhamishaji fedha.

Viashiria vingine ni shughuli za kilimo, makazi ya kaya na upatikanaji wa maji, matumizi na usalama wa chakula katika kaya, maamuzi katika kaya, ukatili kwa wanawake na matarajio ya vijana, mahusiano ya kaya na jamii pamoja na mtazamo wa kaya kuhusu Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Utafiti wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania wa awamu ya pili utahusisha kaya takribani 7,000 ambazo zilihojiwa katika utafiti wa awamu wa kwanza uliofanyika Juni, 2015.