Serikali yaahirisha mnada wa tanzanite

SERIKALI imeahirisha mnada wa Madini ya Tanzanite uliokuwa ufanyike kuanzia Oktoba 12 hadi 15, mwaka huu katika mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano serikalini, ilisema Wizara ya Madini inatoa taarifa kwa umma kuwa Mnada wa Madini ya Tanzanite uliokuwa ufanyike katika mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro mkoani Manyara kuanzia Oktoba 12 hadi 15, mwaka huu, umeahirishwa hadi hapo utakapotangazwa tena.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sababu ya kuahirishwa kwa mnada huo ni kuridhia maombi ya wadau wa mnada ambao waliomba kupata muda zaidi wa maandalizi ili wapate fursa ya kushiriki kwa wingi na kwamba uongozi wa Wizara na Mkoa wa Manyara watapata muda zaidi wa kuandaa mazingira salama na bora zaidi ya kufanyia mnada huo katika mji wa Mirerani.