TRA yaonya bidhaa za magendo

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa onyo kwa wafanyabiashara wanaokwepa kodi na kuingiza bidhaa za magendo kupitia viwanja vya ndege, vituo vya forodha mipakani, njia za panya na bandari bubu nchini wakae chonjo.

Kamishna Mkuu wa TRA nchini, Charles Kichere amesema katika taarifa yake kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara atakayebainika kusafirisha bidhaa kwa magendo na kukwepa kodi nchini.

Amewataka wafanyabiashara hao kuacha mara moja vitendo hivyo vinginevyo mali zao zote zitakazokamatwa na chombo kilichotumika kusafirisha au nyumba iliyohifadhi bidhaa hizo zitataifishwa na serikali kufidia ukwepaji kodi.

Kichere alisema kukwepa kodi ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2005 na Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015.

Alisema ukwepaji kodi husababisha mambo mengi ikiwemo kuikosesha serikali mapato.

Kichere alisema ukwepaji kodi huhatarisha maisha ya walaji kwa kuingiza bidhaa ambazo hazijathibitishwa viwango vya ubora na usalama wake kupitia mamlaka husika kama Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), lakini pia huhatarisha uchumi na usalama wa nchi kwa sababu ya kuweza kuingiza vitu vya hatari kama silaha.

TRA imewataka wananchi kutoa taarifa ya mfanyabiashara au kampuni inayojihusisha na magendo na kukwepa kodi kwa kupiga simu namba +255 22 2137638 au +255 784 210209.

Hivi karibuni TRA ilitaifisha tani moja ya sukari na chumvi, majani ya chai mifuko 18, mirungi kilogramu 16, vifaranga vya kuku 5,000 na mayai kasha 416 mpaka wa Namanga, Arusha zikitokea Kenya kwa njia zisizo rasmi.