Deni La Rwanda linalipika-IMF

SHIRIKA la Fedha Duniani (IMF) limesema licha ya kiwango cha deni la taifa kuwa kubwa kwa miaka iliyopita, nchi hiyo ina uwezo wa kulilipa. Mkuu wa IMF, Laura Redifer alisema kuna wakati nchi inahitaji kukopa ili iweze kukua kiuchumi.

"Deni la Rwanda linalipika, nchi inatakiwa kuwa na deni ili kukua,wizara ya fedha iko makini kwa aina ya madeni inayokopa , jambo kubwa tunalotakiwa kuwa makini ni madeni hatari,” alisema.

Alisema kati ya nchi za Afrika, zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, madeni yamekuwa yakiongezeka kwa sababu mbalimbali na kwamba kuna baadhi ya nchi zikiwemo za Afrika Mashariki zimekuwa zikichukua mikopo mingi kwa ajili ya miundombinu.

Alisema Rwanda imekuwa ikichukua mikopo kwa kuzingatia jinsi wanatumia na pia kurejesha ambapo kiwango cha mikopo kimeongezeka katika miaka michache iliyopita lakini wanaamini watalipa.

Kwa mujibu wa wizara ya fedha, mipango na uchumi kiwango cha deni la nje na pato la ndani ni asilimia 36.6 ambalo ni dogo kwa nchi za Afrika Mashariki kwa asilimia 50 huku deni la ndani likiwa asilimia 10 mwishoni mwa mwaka 2017.

Alisema deni hilo limeongezeka kulingana na mwaka 2016 ambapo deni la nje na pato la ndani lilisimama kwa asilimia 35.2 wakati deni la ndani likiwa asilimia 9.4.