Nidhamu, weledi vimeimarisha jeshi letu-Balozi Seif

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema nguvu na sifa za kiulinzi zilizojengeka ndani ya Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania katika nyanja za kimataifa itabaki kuwa historia endapo nidhamu ndani ya majeshi hayo itaendelea kuwa ya kudumu.

Alisema nidhamu na weledi ndivyo vigezo pekee vikubwa vilivyoufanya Umoja wa Mataifa kuyaamini majeshi ya Tanzania katika ulinzi wa amani katika nchi zenye migogoro na vita ya wenyewe kwa wenyewe hasa barani Afrika hivyo, lazima mambo hayo yasimamiwe kwa nguvu zote.

Alisema hayo wakati akizungumza na Mkuu Mpya wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Venance Mabeyo aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli ambaye aliyefika ofisini kwake Vuga mjini Unguja kujitambulisha rasmi.

Alisema umahiri wa majeshi hayo katika ulinzi wa kitaifa na kimataifa; pamoja na ulinzi wa raia na mali zao, umeyafanya kuaminika kiasi cha kuwa faraja kwa wananchi na mataifa wanayopangiwa kusimamia ulinzi wa amani.

Balozi Seif aliwashauri wananchi kujiepusha na tabia ya kuyatumia maeneo yaliyo karibu na kambi za ulinzi kwa kujenga nyumba za makaazi ya kudumu au kulima ili kujikinga na hitilafu zinazoweza kutokea za milipuko ya silaha nzito ambazo baadaye huleta athari za kiafya au wakati mwingine vifo.

Mabeyo aliyeteuliwa na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo Februari mwaka huu, alisema majeshi ya Tanzania yataendelea kuwajali na kuwaheshimu wananchi kwani wao ni sehemu ya majeshi hayo.