Nape kutembelea Clouds kupata mzizi wa uvamizi

WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye leo anatarajia kutembelea Kituo cha Habari cha Clouds Media ili kujua kilichotokea kutokana na madai kuwa kituo hicho kilivamiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni askari wenye silaha.

Katika taarifa aliyoitoa kwenye ukurasa wake wa Tweeter, Nape alithibitisha kwamba atatembelea kituo hicho leo ambacho katika uvamizi huo, inadaiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitajwa kuonekana kuwaongoza askari hao.

“Nawaomba wanahabari wote nchini na vyombo vya habari kuwa watulivu,” alisisitiza waziri huyo.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Clouds Media umetoa taarifa kuhusu suala hilo ukieleza kwamba kumekuwa na habari kuhusu Clouds Media Group na viongozi mbalimbali akiwamo Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na Mkuu wa Mkoa, Makonda.

“Kiini cha habari hizo zote ni uwepo wa taarifa zinazomhusu mwanamke anayedai kuzaa na Askofu Josephat Gwajima,” ilifafanua taarifa ya Clouds Media Group. “Pamoja na ukweli wa mengi ya matukio hayo, jambo hili lipo katika uchunguzi wa kina unaofanywa na sisi Clouds Media Group kwa kushirikiana na mamlaka zote zinazohusika. Tunaomba radhi kwa madhara yoyote na jambo hili na tunawaomba Watanzania wote kutupa muda zaidi kabla ya kutoa tamko rasmi kuhusu yote yaliyotokea,” iliongeza taarifa hiyo.

Awali, Askofu Gwajima alibainisha kuwa tuhuma zinazosambazwa kuwa amezaa na mmoja wa waumini wake, si za kweli kwani mwanamke anayehusishwa naye pamoja na kuwa na tatizo la afya ya akili, lakini pia ana mume wake.

Gwajima aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akihutubia kanisani kwake na kusisitiza kuwa, taarifa hizo zimezushwa na kusambazwa kwa lengo la kuzima suala la utata wa vyeti vya taaluma linalomkabili Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Alikiri kumfahamu mwanamke huyo ambaye video yake imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii akikiri kuwa amepewa mimba na kuzaa na askofu huyo, na kubainisha kuwa anaishi jirani na Kanisa hilo la Ufufuo na Uzima.

“Mnamkumbuka yule mwanamke aliyeolewa na Said Amiri Kipingu ambaye ana tatizo la akili (afya). Sasa huyu mwanamke amekuwa leo stori katika jiji hili, nyumbani kwao ni hapa jirani na kanisa hili, baba yake mzazi nimeongea naye jana (juzi),” alidai Gwajima.

Mtumishi huyo wa Mungu alimtuhumu RC Makonda kuwa ndiye aliyemchukua mwanamke huyo bila kujua kama ana tatizo la afya ya akili na kumlisha maneno ya kumchafua Askofu huyo.

“Na baba wa mwanamke huyu na mume wake kesho (leo) watakuja hapa kanisani kutoa ushahidi, mimi ni mtumishi wa Mungu nasema ukweli,” alisisitiza.

Alielezea namna mwanamke huyo alivyochukuliwa kwa ajili ya kurekodiwa na kushurutishwa atoe tuhuma za kuwa na uhusiano na kuzaa na mchungaji Gwajima bila watu waliomchukua kufahamu kuwa ni mgonjwa wa afya ya akili.

Aidha, alisema katika tuhuma hizo za kuzaa na mwanamke huyo, vielelezo vilivyotolewa vinatia shaka kwani hata cheti za kuzaliwa cha mtoto anayedaiwa kuwa ni wake kina mapungufu zaidi ya 10 yanayoibua shaka kuwa suala hilo, limetengenezwa.

Alisema cheti husika hakina jina la hospitali, mahali wanakoishi wazazi, mhudumu aliyemzalisha mwanamke huyo, hakina muhuri pamoja na mahali alikozaliwa mtoto husika.

Pamoja na hayo Askofu Gwajima alitoa tuhuma kali dhidi ya RC huyo wa Jiji la Dar es Salaam ikiwemo cheti cha matokeo ya kidato cha nne cha mtu anayeitwa Daudi Bashite ambacho mtumishi huyo wa Mungu alidai ni cha RC huyo.

Hata hivyo, RC Makonda tangu kuanza tuhuma za kutumia cheti cha mtu mwingine amekuwa akitupilia mbali madai hayo na kusisitiza kuwa yamekuwa yakitolewa kwa lengo la kuzima mapambano dhidi ya dawa za kulevya aliyoyaanzisha hivi karibuni.