Wanazuoni wagongana matumizi ya Kiswahili

WASOMI nchini wameendelea kuvutana kwa hoja kuhusu suala la kuitumia lugha ya Kiswahili katika shughuli mbalimbali ikiwemo kufundishia, huku baadhi yao wakisisitiza lugha hiyo haijitoshelezi na wengine wakisisitiza ianze kutumika kwa kuwa hakuna lugha yoyote duniani iliyojitosheleza.

Katika mjadala huo, Balozi wa Kwanza wa Kiswahili Afrika, Mama Salma Kikwete amebainisha kuwa pamoja na upungufu uliopo kwenye lugha hiyo ya Kiswahili, bado inaweza kutumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo kufundishia huku uwekezaji wa kuikuza na kuipanua ukiendelea.

Akizungumza katika Kongamano la Matumizi ya Lugha ya Kiswahili kwenye Ukumbi wa Nkrumah katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana, Mama Salma alisema kihistoria lugha ya Kiswahili imekuwa na mchango mkubwa nchini kutokana na kutumika katika harakati za ukombozi, lakini pia kuwaunganisha Watanzania na kuwafanya wamoja.

Alisema pamoja na kwamba watanzania wanatumia lugha nyingine za asili, lakini lugha yao ya pili ni Kiswahili na ni wachache ache hawaifahamu lugha hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukua nje ya nchi.

Alisema hakuna sababu yoyote inayoweza kutolewa na kuifanya lugha hiyo isitumike kufundishia kwani kama suala ni kutojitosheleza, hakuna lugha yote duniani iliyojitosheleza na lugha zote zimekopa maneno kutoka kwa lugha nyingine.

Aliwapongeza marais wa awamu zote kwa mchango wao wa kukuza Kiswahili akiwemo Rais wa Awamu ya Kwanza hayati Julius Nyerere, Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ya Tatu, Benjamin Mkapa, ya Nne Jakaya Kikwete na wa sasa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.

Kwa upande wake, Mhadhiri na mtaalamu wa lugha ya Kiingereza, Dk Michael Kadeghe, alisema bado Kiswahili hakina hadhi ya kuanza kutumika kufundishia kwa kuwa hakijitoshelezi katika nyanja nyingi ikiwemo istilahi na lahaja.

Alitahadharisha na kuitaka serikali iwe makini na uamuzi wake katika suala la lugha ya kufundishia kwani ki ukweli bado lugha hiyo ni lugha ya pili kwa watanzania wengi lakini pia lugha hiyo haiendani na taaluma hasa zile za kisayansi.

“Mwaka 1982 aliyekuwa Waziri mkongwe hapa nchini, Jackson Makweta aliwahi kutamka kuwa Kiswahili kitumike kuwa lugha ya kufundishia sekondari lakini mwaka uliofuata alipochaguliwa kuwa waziri wa elimu alifuta kauli yake na kukiri kuwa alikosea na kutangaza kiingereza kiendelee kufundishia sekondari,” alisisitiza Kadeghe.

Naye Katibu Mkuu anayeshughulikia Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda alisema bado lugha hiyo inahitaji uwekezaji wa kutosha katika kukuzwa na kupanuliwa na endapo itatumika kama ilivyo katika kufundishia kuna hatari kubwa ya kuzalisha taifa la watu wasioelewa vyema taaluma zao.

“Kwa mfano udaktari au uhandisi, taaluma hizi zina istilahi zake sasa nina uhakika mpaka sasa Kiswahili chenyewe hakijafanikiwa kutafuta baadhi ya maneno katika sekta mbalimbali za kisayansi zilizopo. Tusipokuwa makini tutatengeneza madaktari watakaouwa wananchi badala ya kuwaponya,” alieleza Profesa Mkenda.

Alisema hata nchi zilizoendelea kama vile Japan, China na Ujerumani zinazotumia lugha zao katika shughuli zote ikiwemo kufundishia zilitumia nguvu kubwa na kuwekeza katika lugha hizo kabla ya kuanza kuzitumia kwenye maeneo yote.

Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwalimu wa somo la Hisabati, Dk Said Sima alisema Kiswahili ndio somo sahihi la kufundishia na kuelezea uzoefu kama mwalimu kuwa wanafunzi wake wengi walielewa na kufaulu pale walipopewa kazi za Kiswahili na kufanya vibaya kwenye kazi za Kiingereza.

Alisema ni vyema lugha hiyo ikapewa nafasi na kuanza kutumika kufundishia ili kujenga kizazi cha wasomi wanaoelewa wanachofunza tofauti na sasa ambapo wengi wao pamoja na kuhitimu bado hawana uelewa wa kutosha juu ya walichojifunza kutokana na tatizo la lugha.