Mabadiliko ya Katiba ya CCM yaondoa tibwiri nafasi ya Urais

MABADILIKO ya Katiba ya CCM yamempa ulaji Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais wa nchi, John Magufuli, kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho 2020 bila kupingwa na mwanachama mwingine ndani ya chama.

Kutokana na mabadiliko hayo, Mwenyekiti wa CCM amepewa ruhusa ya kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho kwa kipindi cha pili bila kupingwa na mwanachama yeyote ndani ya chama isipokuwa atashindana na wagombea wa vyama vya upinzani.

Hivyo, kama kulikuwa na mwanachama yeyote mwenye nia au ndoto za kuomba au kuwania nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao wa 2020, asubiri baada ya mwenyekiti wa sasa kumaliza kipindi cha pili, labda asubiri 2025.

Mabadiliko hayo yaliyopitishwa na Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliofanyika Machi 12, mwaka huu, kwenye Ukumbi wa Kikwete mjini Dodoma yaliridhiwa kwa kauli moja na wajumbe wote wa mkutano huo.

Katiba itakayotolewa baada ya marekebisho haya itakuwa toleo la 13 katika mabadiliko ambayo wakuu wa chama hicho tawala wamesema yamelenga muundo, mfumo, uongozi na utendaji wa viongozi wa chama tangu ngazi ya shina hadi Taifa.

Kabla ya mabadiliko hayo ya karibuni, CCM ilikuwa inaruhusu mwanachama wake yeyote kujitokeza kuwania urais hata wakati wa muhula wa kwanza wa urais unapomalizika kwa rais aliyeko madarakani, ambaye kwa miaka yote tangu Uhuru ametokana na chama hicho kikongwe nchini.

Aidha, katika mkutano wa Machi 12, ulioongozwa na Mwenyekiti wake, Dk Magufuli uliridhia kwamba kura za maoni za wabunge zipigwe na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo badala ya utaratibu wa zamani wa kupiga wanachama wote.

Vile vile kura za maoni za madiwani zitapigwa na Mkutano Mkuu wa Kata na sio wanachama wote kama ilivyokuwa katika Katiba ya CCM ya 1977 Toleo la 2012.

Marekebisho ya upigaji kura yanalenga kudhibiti taratibu za kura za maoni majimboni, kuepusha migawanyiko, kuziba mianya ya rushwa na kuepusha wapigakura mamluki.

Mabadiliko ambayo yaliyosomwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kabla ya Mwenyekiti Magufuli kuuliza wajumbe wa mkutano kuyaridhia, alisema yanalenga kupunguza vikao vya uamuzi kutokana na gharama kubwa za kuviendesha.

Pamoja na kupunguza vikao vya uamuzi, pia yanalenga kupunguza wajumbe mikutano katika ngazi mbalimbali ukiwamo Mkutano Mkuu wa CCM kutoka wajumbe 2,422 hadi 1,706 ambapo wajumbe waliobaki ni sawa na asilimia 70.4.

Aidha, wajumbe wa Halmashauri Kuu wamepunguzwa kutoka 388 hadi 163 ambao wamebaki wajumbe asilimia 40.01, pungufu ya nusu ya wajumbe wote.

Wakati wajumbe wa Kamati Kuu (CC) wemepungua kutoka 34 hadi 24 ambao ni sawa na wajumbe asilimia 70.6 waliobaki na kufanya idadi ya wajumbe waliondolewa kwenye vikao vitatu vya uamuzi kufikia theluthi moja ya wajumbe sawa na asilimia 33.43.

Kinana alisema, chama kimepunguza wajumbe katika ngazi za juu, ili kukirudisha chama kwa wananchi, au kwenye ngazi za chini ambako kuna wapiga kura.

“Uzito mkubwa umewekwa katika kuimarisha chama katika ngazi ya shina, eneo ambalo wapo wapigakura, kwa kufanya hivyo, chama kitakuwa karibu na watu, watakiona ni chama chao,” alisema Kinana.

Wajumbe wa mkutano huo maalumu waliridhia kwamba, wajumbe wa NEC watakuwa wanatokana na mikoa si wilaya kama ilivyokuwa awali, hivyo kila mkoa utakuwa na M-NEC mmoja, ikimaanisha kwamba hakuna tena MNEC wa wilaya.

Marekebisho hayo katika Ibara ya 61(d) yanaonesha kwamba wajumbe waliokuwa wanaingia katika mikutano hiyo kama makatibu wa fedha na uchumi kuanzia ngazi ya tawi hadi mkoa wamefutwa sambamba na makatibu wasaidizi wa mikoa na wilaya.

Katika futafuta hiyo, Kinana alitangaza kwamba wajumbe wawili wa kuchaguliwa kwenye kamati za siasa za mikoa na wilaya wamefutwa.

Mabadiliko hayo pia yamelikumba shirikisho la vyuo vikuu au mkoa wa vyuo vikuu wa CCM, ambayo ilikuwa taasisi inayojitegemea, sasa itakuwa Idara ya UVCCM na itawajibika chini ya jumuiya hiyo ya chama.

Lengo la mabadiliko hayo, kwa mujibu wa Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole ni kukirudisha chama kwa wananchi, lakini pia ni kuongeza ufanisi na utendaji wa viongozi wake.

Pia ni kuzima tabia ya viongozi wachache kujilimbikizia nafasi nyingi za uongozi zenye kazi ya muda wote, ambao hushusha ufanisi na kupunguza tija.