Zanzibar yapumua deni la Tanesco

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewatoa hofu wananchi wa Zanzibar kuwa hawatokatiwa umeme baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuanza kulipa deni inayodaiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Tayari SMZ imelipa jumla ya Sh bilioni 10 kati ya Sh bilioni 127.87 ambazo Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) linadaiwa na Tanesco. Hayo yalibainishwa katika mazungumzo yaliyofanyika baina ya Rais John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Ikulu, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Profesa Muhongo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Tanesco, Kahitwa Bishaija na Meneja Mwandamizi wa Fedha wa shirika hilo, Sadock Mugendi.

Akizungumzia deni la SMZ katika Tanesco, Profesa Muhongo alisema pamoja na kiasi hicho cha Sh bilioni 10 kilichokwishalipwa, SMZ itaendelea kulipa deni hilo mpaka litakapomalizika.

Aidha, alitoa mwito kwa wadaiwa sugu wote wa Tanesco kulipa madeni yao katika kipindi cha siku tano zilizobaki kwa kuwa wasipolipa watakatiwa umeme.

Hivi karibuni, Tanesco ilitoa siku 14 kwa wateja wake wote inaowadai kulipa madeni yao, vinginevyo itawakatia huduma ya umeme wateja wote sugu inaowadai.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, alisema shirika hilo linadai jumla ya Sh bilioni 275.38.

Mkurugenzi huyo aliwataja wadaiwa sugu wa shirika hilo kuwa ni Wizara na Taasisi za Serikali zinazodaiwa zaidi ya Sh bilioni 52.53, Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) linalodaiwa zaidi ya Sh bilioni 127.87 na kampuni binafsi pamoja na wateja wadogo ambao deni lao ni zaidi ya Sh bilioni 94.97.