Magufuli kuweka jiwe la msingi barabara ya juu Ubungo

RAIS John Magufuli leo anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Ubungo ambao utagharimu zaidi ya Sh bilioni 188.71, na kusaidia kuondoa tatizo kubwa la foleni katika Jiji la Dar es Salaam.

Mradi huo ni kati ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi waliyoiahidi wakati wa kampeni ukiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya juu Tazara, ujenzi wa bomba la mafuta, ujenzi wa reli ya kisasa, ununuzi wa meli katika maziwa makubwa nchini, na mengine mengi.

Uzinduzi wa mradi huo ambao umelenga kupunguza msongamano wa magari katika barabara za Morogoro, Nelson Mandela na Sam Nujoma, pia utahudhuriwa na Rais wa Benki ya Dunia, Dk Jim Yong Kim aliyetarajiwa kuwasili nchini jana kwa ziara ya siku tatu nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ilieleza kuwa mradi huo ni sehemu ya mradi wa uboreshaji usafiri jijini Dar es Salaam, utakaogharimiwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia na mchango wa Serikali ya Tanzania.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba mradi huo utahusisha pia awamu ya tatu na ya nne ya ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (Bus Rapid Transit- BRT), katika barabara ya Nyerere kutoka katikati ya Jiji hadi Gongo la Mboto na barabara ya Bagamoyo kutoka katikati ya Jiji hadi Tegeta.

Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema zaidi ya magari 65,000 yanapita kila siku katika makutano ya barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma eneo la Ubungo hali inayosababisha msongamano katika barabara ya Morogoro ambayo ndio lango kuu la kuingia na kutoka jijini Dar es Salaam.

Mfugale alisema kulingana na usanifu, barabara za juu katika eneo la Ubungo zitajengwa kwa safu tatu, ambapo safu ya chini itatumika kwa magari yanayopita katika Barabara ya Morogoro pamoja na magari yote yanayopinda kushoto.

Alisema safu ya pili itajengwa katika utefu wa meta 5.75 kutoka usawa wa ardhi na itatumika kwa magari yote yanayopinda kulia ambayo yataongozwa pia na taa za barabarani; wakati safu ya tatu itajengwa kwa urefu wa meta 12.5 kutoka usawa wa ardhi na itatumika kwa magari yanayopita barabara ya Mandela na Sam Nujoma na barabara zote zitakuwa na njia sita za magari ikiwa ni pamoja na njia mbili za magari ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka.