Mbunge ataka fursa za Kigamboni zitangazwe

MBUNGE wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile ametoa mwito kwa wanahabari kuitangaza wilaya hiyo ambayo bado ni mpya kwa kuelezea vivutio na fursa zinazopatikana katika wilaya hiyo ili ikue kwa kasi.

Dk Ndugulile aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mkutano wake na waandishi wa habari wanaoishi Kigamboni ambapo pia uliwashirikisha viongozi wa wilaya hiyo lengo likiwa ni kujenga ukaribu, uhusiano na mfumo wa mawasiliano.

“Tuna kazi kubwa sana ya kuitangaza wilaya yetu, tunapaswa kuelezea umma ni fursa zipi zinapatikana Kigamboni na vivutio gani vipo… hii itasaidia kukuza wilaya yetu,” alisema mbunge huyo wa Kigamboni.

Aidha, alisema amedhamiria kuhakikisha wilaya hiyo inakuwa katika kila sekta ambapo kwa upande wa sekta ya elimu amedhamiria kuweka umeme katika shule zote za sekondari ambazo hazina umeme kwa kupitia fedha za mfuko wa jimbo lengo likiwa ni kukuza kiwango cha elimu.

Alisema kwa upande wa huduma za afya alisema wamehakikisha kwamba dawa zinapatikana katika zahanati, vituo vya afya na hospitali huku wakiendelea na mikakati ya kujenga hospitali ya wilaya hiyo.

Mkuu wa wilaya hiyo, Hashim Mgandilwa alisema wameandaa dokumentari ambayo itabeba fursa zote zilizopo Kigamboni lengo likiwa ni kuitangaza wilaya hiyo.

Mgandilwa alisema kuna changamoto kubwa ya elimu lakini kwa sasa wanazishughulikia ili kuhakikisha wilaya hiyo inaongoza katika mitihani ya Taifa.

Mapema Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Rahel Mhando aliwaasa wanahabari kuzingatia maadili na misingi ya taaluma sanjari na kuimarisha ushirikiano ili kuleta matokeo chanya katika kuitangaza Kigamboni, moja ya wilaya mpya nchini zilizoanzishwa hivi karibuni.