Utafiti wa viashiria vya Ukimwi wazinduliwa Kilimanjaro

SERIKALI mkoani Kilimanjaro imewaomba wananchi katika kaya zilizopendekezwa kushiriki katika utafiti wa viashiria kuhusu maambukizi mapya ya Ukimwi, magonjwa ya homa ya ini na kaswende kutoa ushirikiano kwa watafiti watakaowatembelea, na utafiti huo hauna malipo.

Akizindua utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania (THIS) Mkoa wa Kilimanjaro, mkuu wa mkoa, Saidi Mecky Sadiki alisema utafiti huo utawahusisha wananchi wa rika zote ikilinganishwa na tafiti tatu zilizotangulia ambazo zilikuwa zikitaja umri maalumu.

“Utafiti huu utaangazia pia uwepo kwa viashiria vya usugu wa dawa, kiwango cha maambukizi ya kaswende na homa ya Ini (Hepatitis B na C) kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 15,” alieleza Sadiki.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa, Sadiki alisema utafiti huo wa 2016/2017, utakusanya taarifa za upatikanaji na utumiaji wa huduma zitolewazo katika kudhibiti maambukizo ya VVU na Ukimwi na viashiria vya tabia hatarishi.