Wagoma kuuza mifugo wakipinga faini

WAFUGAJI zaidi ya 1,400 kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora wamegoma kuuza mifugo yao ya ng’ombe na mbuzi baada ya wenzao kukamatwa na kutozwa faini ya Sh 50,000 na Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.

Watu hao walitozwa faini baada ya kupitisha mifugo yao katikati ya mji, ikiwa ni pamoja na kuharibu miundombinu ya barabara zinazoendelea kutengenezwa kwa kiwango cha changarawe.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki mnadani hapa, baadhi ya wafugaji na wafanyabiashara wa ng’ombe na mbuzi, Gandu Daudi, Ndila Kasembe, na Sitta John ambaye ni mwenyekiti wao, walidai kilichowashangaza ni kuona wanakamatwa na mgambo wa halmashauri hiyo huku wakitozwa faini ya Sh 50,000 pasipo kuoneshwa maeneo ya malisho na sehemu maalumu za kupitishia mifugo yao wanayopeleka kuuza mnadani kila Jumamosi.

Gandu alisema maeneo yaliyokuwepo zamani ya kupitisha mifugo wakati wakipeleka mnadani baadhi yake yamelimwa mazao ya mahindi na wakulima huku maeneo mengine yakiwa katikati ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Igunga, jambo ambalo wamedai wamekuwa wakipata shida kupeleka au kuitoa mifugo yao kwenye mnada huo.

Pamoja na malalamiko hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Igunga, Revocatus Kuliza alisema kwamba hayuko tayari kuvunja sheria kwa kuwa Igunga ni Mamlaka ya Mji Mdogo hivyo mifugo hairuhusiwi kupitishwa katikati ya mji kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi.

Alisema maeneo ya kupitisha mifugo yao ilishatengwa na viongozi waliomtangulia hivyo alishangazwa kuona wakilalamikia sehemu hizo na kusema ataendelea kutoza faini kwa mifugo inayokatisha na kuzurura hovyo katikati ya mji.

Hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakati wa kampeni ya upandaji miti wilayani Igunga alipiga marufuku mifugo kuzurura mjini, ikiwa ni moja ya kudhibiti uharibifu wa miti na mazingira kwa ujumla, jambo ambalo wafugaji wameendelea kukaidi.