Mara wazindua mradi wa REA lll

SERIKALI imezindua mradi kabambe wa kupeleka umeme vijijini awamu ya tatu katika Mkoa wa Mara, kwa kumtaka mkandarasi aliyepewa kazi hiyo, Kampuni ya Angelique International Limited kutekeleza mradi huo kwa wakati uliopangwa kulingana na mkataba uliopo ili kuwaondolea wananchi kero ya umeme.

Mradi huo umezinduliwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani katika Kijiji cha Mariwanda wilayani Bunda.

Akizindua mradi huo wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu, Dk Kalemani alisema mradi huo utagharimu zaidi ya Sh bilioni 41.15 na kwamba vijiji na vitongoji vyote vya Mkoa wa Mara vitapata nishati hiyo ya umeme, hali itakayoharakisha maendeleo ya wananchi.

Aidha, alitoa maelekezo kwa mkandarasi huyo kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa wa miaka miwili na kwamba umeme huo, hakuna kuruka kijiji hata kimoja na kuongeza kuwa mkandarasi pia afanye kazi kwa saa 24, na pia awalipe kwa wakati vibarua atakaokuwa amewaajiri katika kazi hiyo.

Alibainisha kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha vijiji vyote Tanzania vinapata nishati hiyo ya umeme ifikapo mwaka 2021.

Akitoa taarifa ya mradi huo wa REA awamu ya tatu, Mkurugenzi katika Wizara ya Nishati na Madini, Gisima Nyamhanga alisema kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) walitekeleza mradi huo kwa awamu ya kwanza vizuri na pia awamu ya pili, ambapo sasa wanaanza kutekeleza awamu ya tatu.

Awali, akisoma taarifa ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Bunda, mkuu wa wilaya hiyo, Lydia Bupilipili alisema jumla ya vijiji 85 vilipata huduma ya umeme kupitia mradi wa REA awamu ya pili, ambako kufikia mwishoni mwa Februari mwaka huu, jumla ya wateja 1,436 waliunganishiwa huduma hiyo.