Ndesamburo atetea walioshindwa kurejesha mikopo

ALIYEKUWA mbunge wa jimbo la Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo ameiomba serikali kuzuia taasisi za fedha kuuza mali za wateja walioshindwa kurejesha mikopo, badala yake waongezewe muda wa kurejesha.

Ndesamburo alitoa ombi hilo jana kwa madai kuwa wafanyabiashara wengi waliokopa wanashindwa kurejesha mikopo yao kwa wakati kwa sababu ya hali ya kiuchumi kwa sasa si nzuri.

Alisema ni vyema serikali iingilie kati suala hili kwa sababu kodi zimekuwa kubwa jambo lililosababisha biashara nyingi kufungwa na nyingine kufilisiwa na taasisi za kifedha kutokana na kushindwa kurejesha mikopo.

“Kama hatua hazitachukuliwa tutaendelea kuongeza umaskini katika nchi na kuna hatari kubwa nchi kurudi nyuma kimaendeleo,” alisema. Alisema serikali inatakiwa kuchukua hatua za makusudi kuweka utaratibu ili taasisi za kifedha zisiuze mali za watu, badala yake wanaodaiwa waendelee kulipa madeni yao taratibu.

“Ni kweli kwamba hakuna biashara, watu wengi wamefilisiwa na benki kutokana na kushindwa kurejesha mikopo, TRA pia kila kukicha wanataka kodi yao hawaangalii umefanya biashara au la!” alisema.

Aidha aliiomba serikali kuchukua hatua kudhibiti matukio mbalimbali ya uhalifu yanayoendelea kufanyika nchini na endapo hatua hazitachukuliwa itahatarisha amani pamoja na maendeleo ya nchi.