Sheria kuondoa VAT vifaa tiba yaandaliwa

SERIKALI inaandaa Sheria mpya ya kutoa msamaha wa kulipia Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa vifaa vya tiba yakiwamo magari ya kubebea wagonjwa.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM) aliyeuliza kwa nini magari ya wagonjwa yanayotozwa (VAT) wakati hayafanyi biashara bali yanatoa huduma.

Dk Kijaji alisema, sheria mpya inayoandaliwa itakapokuja itakuwa na ufumbuzi wa suala hilo la vifaa tiba na magari ya huduma za wagonjwa kupewa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani.

Akijibu swali la Mbunge wa Mafinga, Cosato Chumi (CCM), aliyetaka kujua ni lini serikali italeta mapendekezo ya sheria ili magari ya wagonjwa yapate msamaha wa kodi, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla alisema sheria ya mwaka 2014, vifaa vya tiba vitapata msamaha baada ya Waziri wa Afya kuridhia.

Dk Kigwangalla alisema, magari ya kubeba wagonjwa ambayo yana vigezo ambavyo vimewekwa, huombewa msamaha wa kodi na waziri mwenye dhamana, hupatiwa msamaha na Wizara ya Fedha na Mipango baada ya kujiridhisha kuwa yana vigezo stahiki.

Kigwangalla alisema katika mwaka wa fedha wa 201/17, wizara haikutengenezwa fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ya wagonjwa na hata katika makadirio ya mwaka huu fedha hazijatengwa.

Alisema, fedha hazijatengwa kutokana na kutambua kwamba ni jukumu la halmashauri husika kunatenga fedha kwa ajili ya kununua magari ya kubebea wagonjwa. Dk Kigwangalla, alisema wizara pindi itakapopata misaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo, imekuwa ikigawa magari haya katika halmashauri mbalimbali nchini kwa kuzingatia mahitaji.