Majaliwa: Tutatoa taarifa ya uchunguzi mauaji na utekaji

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waiamini serikali yao kwamba inafanya uchunguzi wa matukio mbalimbali yaliyotokea nchini hivi karibuni ya kutekwa, kukamatwa na kuuawa askari wanane, ikikamilisha ripoti itatolewa.

Kauli hiyo ya msisitizo alitoa bungeni jana wakati Waziri Mkuu, Majaliwa akijibu swali la papo kwa hapo la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Chadema) aliyetaka kusikia kauli ya serikali kuhusu matukio ya utekaji watu na mauaji ya askari yaliyotokea hivi karibuni na kuzua taharuki miongoni mwa wananchi.

Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai alisema, kumekuwa na hali ya mashaka siku za hivi karibuni ambayo imeibua hofu miongoni mwa wananchi kutokana na watu kutekwa, kupotea na askari kuuawa, akatoa mfano wa Ben Saanane ambaye ni miezi sita tangu amepotea serikali haijatoa kauli yoyote.

Waziri Mkuu, Majaliwa alisema: “Watanzania wanatakiwa kuwa na imani na serikali yao kwamba inafanya uchunguzi wa uhakika, ikikamilisha itatoa taarifa kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali,” alisema.

Majaliwa alisema jambo hilo la upoteaji, utekwaji na kuuawa kwa askari, alitoa taarifa ya awali wakati akihitimisha bajeti ya ofisi yake, hata hivyo kinachotakiwa ni wananchi kuwa na imani na serikali yao kwamba inafanya uchunguzi na itatoa taarifa.

Waziri Mkuu alisisitiza kwamba pia Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alitoa taarifa kwa wabunge mwanzoni mwa wiki hii kuhusu kuuawa kwa askari kwamba vyombo vya usalama vinaendelea kufanya uchunguzi, kinachotakiwa ni Watanzania kuvipa muda vyombo vya uchunguzi ili kukamilisha uchunguzi huo.

Alisema pamoja na kutolewa kwa taarifa hiyo, bado wabunge wamekuwa wakitoa michango ya hoja bungeni wakitaka kusikia kauli ya serikali kuhusu mambo hayo, “Ila nachoomba waendelee kuwa na imani na vyombo vya uchunguzi kwamba vinaendelea na kazi hiyo, vikikamilisha taarifa itatolewa.”

Majaliwa alisema jukumu la serikali ni kutumia vyombo vya ulinzi na usalama na kuhakikisha kwamba wananchi wanapata ulinzi na usalama wao wenyewe na mali zao, na serikali itahakikisha inaimarisha ulinzi huo.

“Wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vinavyofanya uchunguzi na kuhakikisha kwamba wahalifu wanapatikana na nchi inaendelea kubaki salama,” alisema. Waziri Mkuu alisema katika kuhakikisha uchunguzi unakuwa wa uhakika na taarifa za uhakika zinapatikana, vyanzo vingi vinatakiwa kusaidia, hivyo akawaomba wananchi waendelee kutoa taarifa mara wanaposhtukia kuwepo kwa hali isiyo ya kawaida katika maeneo yao.

Kuhusu swali la nyongeza la Mbowe la kuomba serikali iombe msaada wa wachunguzi wa nje kama Scotland Yard ya Uingereza, Waziri Mkuu alisema serikali ina uhusiano mzuri na taasisi nyingi katika kufanya masuala mbalimbali likiwamo la uchunguzi.

Majaliwa alisema serikali inaendelea kufanya uchunguzi kwa kutumia wataalamu wake wa ndani, haijakwama katika uchunguzi na ukikamilika jamii itajulishwa, kinachotakiwa wanatakiwa kuwa watulivu wakati huu.

Kuhusu suala la Ben Saanane kupotea miezi sita na serikali kutota taarifa, Waziri Mkuu aliahidi kwamba vyombo vinavyohusika vitatoa taarifa na familia yake itajulishwa kuhusu jambo hilo.

Kuhusu kurushwa Bunge live, Waziri Mkuu alisema, utaratibu wa matangazo ulioandaliwa unaendelea kutumika na kufuatwa na Watanzania wanapata habari hizo, hata hivyo utaratibu huo unaendelea kuboreshwa.

Kiongozi wa upinzani aliuliza swali hilo akigusa matukio ya kutekwa waandishi katika studio ya Clouds, kutekwa kwa msanii Roma Mkatoliki na kuuawa kwa askari wanane eneo la Kibiti pamoja na kupotea kwa msaidizi wa Mbowe, Saanane miezi sita iliyopita.