Hakuna ndoa ya muda maalumu -Rita

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), umesema hakuna ndoa ya muda maalumu, ndoa ya jinsia moja wala ya mkataba kwa kuwa ndoa ni muungano wa hiyari kati ya mwanamume na mwanamke unaokusudiwa kudumu kwa maisha yao yote.

Ofisa Usajili, Kitengo cha Ndoa na Talaka, Jane Barongo alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na HabariLeo jijini Dar es Salaam. Barongo alisema ndio maana wafunga ndoa wanapaswa kuzingatia vigezo halali vya uhalali wa ndoa ikiwemo umri unaokubalika kisheria kuanzua miaka 18.

Alisema kigezo kingine ni kufunga ndoa kwa hiyari yao na sio kulazimishwa, kusiwepo na pingamizi lililowekwa kuhusu ndoa kabla haijafungwa na pia ifungwe na mtu aliye na mamlaka ya kufungisha.

“Ndoa ya kiserikali hufungwa na wakuu wa wilaya na makatibu tawala wa wilaya, ya kidini hufungishwa na viongozi wa kidini wenye leseni hai na ndoa za kimila ifungwe mbele ya ofisa tarafa,” alisema.

Alisema baada ya kufunga ndoa, wanandoa wanapaswa kupata cheti cha ndoa ambacho kitatoa utambulisho kwa wanandoa. Pia humpatia mwanandoa haki za kumrithi mwenzi wake anapofariki dunia pamoja na kupata haki mbalimbali zinazotolewa na mwajiri wa mwenzi wake.