Takukuru yaokoa mil 74/- semina hewa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Arusha imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh milioni 74.8 zilizolipwa kwa watumishi na semina hewa. Aidha watumishi wa umma wamesisitizwa kufanya kazi kwa maslahi ya umma, kwa kuzingatia suala zima la uadilifu na kuacha kuwashawishi wananchi kutoa fedha ili wapate huduma.

Hayo yalisemwa jana na Kaimu Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Arusha, Frida Wikessy wakati alipotoa taarifa ya utendaji kazi wa tasisi hiyo katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu.

Wikessy alisema fedha hizo zimerejeshwa serikalini baada ya kuziokoa kutokana na watumishi hewa pamoja na semina hewa zilizoandikwa kwa kughushi saini ili watu wajipatie fedha. Alisema fedha hizo zilitokana na watumishi hewa Idara ya afya na elimu ambapo kulikuwa na watumishi wameacha kazi, kufa na wengine kuhama vituo vya kazi, lakini serikali iliendelea kulipa.

Aidha katika kipindi hicho mkoa huo ulipokea jumla ya malalamiko 248 kwa njia mbalimbali na kati ya hayo majalada 24 ya uchunguzi yanaendelea, yapo katika hatua mbalimbali. Frida alisema katika uongozi wa awamu ya tano umekuwa na ongezeko la wananchi kutoa taarifa nyingi tofauti na miaka ya nyuma, hali inayosababisha kupokea malalamiko yalio sahihi na yasio sahihi. Pia alisema katika kipindi hicho mashauri 14 yalisikilizwa na kati ya hayo 10 yalishinda katika kesi za jinsi na uhujumu uchumi.