Mawaziri EAC wataka mfumo mmoja wa elimu

BARAZA la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) limejadiliana kuhusu kuwepo kwa mfumo wa elimu utakaotoa nafasi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu katika nchi wanachama kusoma nchi yoyote kwa mfumo na gharama zinazofanana bila vikwazo.

Wakati huohuo, ikiwa imebaki miaka miwili kabla ya kusitishwa kuagizwa kwa nguo za mitumba, baraza hilo limejadiliana kama viwanda vya nchi wanachama viko tayari kwa uzalishaji wa nguo za kutosha.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Augustine Mahiga wakati akizungumza na wanahabari nje ya mkutano wa 34 wa baraza hilo jana jijini Dar es Salaam. Dk Mahiga alisema, zamani kulikuwa na Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki ambacho kilikuwa na vyuo tanzu katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, lakini kutokana na maendeleo, baadaye kila nchi ilikuwa na vyuo vikuu vyake.

“Tunaona kuna umuhimu wa kuwa na mfumo wa elimu ambao utatoa nafasi kwa wanafunzi wetu kuhudhuria masomo na mafunzo katika nchi zetu kwa malipo yanayofanana, taratibu zinazofanana na vigezo vya kuingia chuo kikuu vinavyofanana,” alisema Dk Mahiga.

Alisema inagawa vyuo vikuu viko katika nchi mbalimbali lakini kusiwepo na vikwazo ambavyo vinaweza kuwakwamisha kusoma katika nchi yoyote ambayo mwanafunzi huyo atapendelea.

“Ukiwa Nairobi na wewe ni Mtanzania unambiwa ulipe kiasi kadhaa na huyu mwingine alipe kiasi kadhaa, tunataka kuondoa hizo tofauti na tutengeze mfumo wa elimu ambao utawezesha vijana wetu kwenda kusoma popote wanapotaka,” alisema.

Dk Mahiga alisema mfumo huo utawawezesha wanafunzi hao wa vyuo vikuu kwenda kusoma mahali kokote na chuo kikuu chochote katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akizungumzia kuhusua suala la nguo za mitumba alisema, wakati Tanzania inachukua uenyekiti wa Jumuiya hiyo, wakuu wa nchi wanachama waliagiza baada ya miaka mitatu, Afrika Mashariki isiagize nguo wala viatu vya mitumba.

Kwa mujibu wa Dk Mahiga, agizo hilo linalenga kutoa nafasi kwa viwanda vya nguo na viatu ndani ya nchi wanachama kufanya vizuri na kuweza kushamiri. Alisema kwa sasa imebaki miaka miwili, hivyo watajadili kama nchi za Afrika Mashariki zina utayari wa kusema mitumba isije na kama wamejipanga vizuri kuzalisha nguo na viatu.

Alisema jambo lingine ambalo watalijadili na kuwasilisha ripoti ya miaka miwili iliyopita Tanzania ikiwa Mwenyekiti kwa Wakuu hao wa nchi ni pamoja na ushirikiano katika biashara, uwekezaji, huduma mbalimbali za uchukuzi kama miundombinu na nyingine pamoja na elimu.

Dk Mahiga alisema, pia watajadiliana kuhusu masuala ya kisiasa ambapo watapeana vipimo na kutazama ushirikiano wa kiuchumi unaleta fursa gani za kusogeza ushirikiano wa kisiasa.

Aidha, alisema kuna uwezekano mkubwa katika kikao cha Wakuu wa nchi za Jumuiya hiyo kitakachofanyika kesho, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa akatoa ripoti ya mchakato wa kuleta mazungumzo ya pamoja na amani nchini Burundi.

Alisema mpaka sasa Marais waliothibitisha kuhudhuria ni wote isipokuwa Sudan ambao wamesema wana udhuru, hivyo watatuma mwakilishi, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Rais wa Rwanda Paul Kagame wote wamethibitisha uwepo wao.

Katika kikao hicho cha 18 kitakachofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais John Magufuli anatarajia kukabidhi uenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa Rais Museveni baada ya muda wake kumalizika.

Alisema Tanzania imechukua nafasi ya uenyekiti wa jumuiya hiyo mara mbili mfululizo, kwani baada ya Mwenyekiti aliyepita Rais Mstaafu Jakaya kikwete kumaliza muda wake, Marais wa nchi wanachama walimchagua Rais Magufuli kuendelea.

“Katika kikao hiki cha 18 mwenyekiti ambaye alikuwa Rais wetu, atampa uenyekiti Rais mwingine ambapo sasa hivi ni zamu ya Uganda, hivyo Rais wetu atakabidhi uenyekiti kwa Rais Yoweri Museveni,” alisema.

Dk Mahiga alisema, baada ya Rais Magufuli kukabidhi uenyekiti huo, Tanzania itakuwa imekamilisha uenyekiti wake kwani yeye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki, ambapo alikabidhi kwa Uganda mwezi Aprili, mwaka huu. Awali, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Kirunda Kivinje alizitaka nchi wanachama kuzingatia jinsi ya kujadili ushirikiano huo kwa mapana na kwa maslahi ya jumuiya hiyo badala ya kukaa na masuala madogo.

Alisema Tanzania na Uganda zinaweza kuwa walishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na kilimo katika sehemu kubwa ya ardhi waliyonayo lakini utasikia watu wanajadili juu ya masuala madogo kama nchi moja watu wake wameajiriwa wengi katika sekretarieti.

“Tumefanya baadhi ya maendeleo, lakini wananchi wetu wanataka matokeo yanayoonekana ili kuboresha ustawi,” alisema Kivinje wakati akiongoza kikao hicho.