Jela miaka 30 kwa kujaribu kumbaka ajuza

MAHAKAMA ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imemuhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, Jovin Bukambo (30) mkazi wa kitongoji cha Nkomolo wilayani humo baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kujaribu kumbaka, Maria Tenganamba(60).

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Ramadhani Rugemalila alisema mahakama hiyo imeridhishwa na ushahidi usiotia shaka yoyote uliotolewa na upande wa mashtaka.

Hakimu Rugemalila alimtia hatiani na kumuhukumu mshtakiwa huyo kutumikia jela miaka 30, kwa mujibu wa kifungu namba 132 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Aliieleza mahakama hiyo kuwa ametoa adhabu hiyo ili iwe fundisho si tu kwa mshitakiwa huyo bali pia kwa wengine wenye tabia kama hizo Awali Mwendesha Mashitaka, Mkaguzi wa Polisi Hamimu Gwelo aliieleza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Oktoba 16 mwaka jana, nyumbani kwa Maria Tenganamba iliyopo katika eneo la Nkomolo wilayani humo saa 11:00 jioni ambapo mtuhumiwa alimvamia mwanamke huyo na kutaka kumbaka.

Alisema akiwa katika jaribio hilo kabla ya kufanikiwa kutenda uhalifu huo mwanamke huyo alipiga kelele za kuomba msaada na kuokolewa na baadhi ya vijana wa kiume waliokuwa karibu na nyumba hiyo, waliofanikiwa kuingia ndani na kumkamata akiwa uchi kisha wakamfikisha katika Kituo cha Polisi.

Upande wa mashitaka uliwaita mashahidi watatu waliotoa ushahidi wao mahakamani hapo ambapo mshitakiwa akijitetea aliiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa kuwa amekaa muda mrefu mahabusu na anategemewa na familia yake