‘Mtanzania hutumia kuni meta za ujazo milioni 50’

KILA Mtanzania hutumia takribani meta moja ya ujazo ya kuni au magogo kwa ajili ya nishati ikiwa ni sawa na zaidi ya meta za ujazo milioni 50 kwa mwaka, Imeelezwa.

Aidha kasi ya uangamizaji misitu nchini inakadiriwa kufikia ekari 372, 000 kwa mwaka huku idadi ya watu nchini imekuwa ikikua kwa takribani asilimia 2.7 kwa mwaka wakati eneo la ardhi haliongezeki.

Hayo yalibanishwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira ) , Ngosi Mwihava ambaye alimwakilisha Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira ) Januari Makamba katika uzinduzi wa mradi wa Jumuiko la Pamoja , Suluhisho la Pamoja (JUPASUPA) uliofanyika jana mjini Sumbawanga mkoani Rukwa .

Mradi huo ni ushirikiano kati ya Serikali ya Uholanzi , Shirika la Kimatiaifa la Uhifadhi wa mazingira la Uholanzi (WWF NL) na Shirika la Kimataifa Kaengesa Rukwa(KAESO).

Ili kuhakikisha uendelevu wa mradi huu hasa katika utekelezaji katika ngazi ya Taifa, asasi zingine zikiwemo HakiArdhi , Action Aid Tanzania (AATZ) na Shirikisho / Timu ya Wanasheria wa Mazingira Tanzania (LEAT) zitashiriki katika mradi huo kwa kusaidiana na serikali katika kuandaa na kutekeleza sera bora na mipango madhubuti ya usimamizi wa ardhi , maliasili na hifadhi ya mazingira katika mikoa ya Rukwa na Katavi.

Alisema kuwa kutokana na uvunaji holela usioendelevu wa maliasili, eneo la ardhi zalishi limekuwa likipungua sana ambapo taarifa ya Mazingira Tanzania imebaini kuwa asilimia 61 ya nchi iko hatarini kuwa jangwa.