Mfuko wa Maji wajazwa fedha

WIZARA ya Maji na Umwagiliaji imeeleza k u a n z i s h w a kwa Mfuko wa Maendeleo ya Maji kumewezesha kupatikana fedha za kutosha ambazo zimeelekezwa katika umaliziaji wa miradi mikubwa ya maji ikiwemo iliyokuwa ikichangiwa na fedha za wahisani.

Mkurugenzi Msaidizi wa wizara hiyo, Jackson Mutazamba alisema hayo juzi mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkakati wa serikali na wizara wa kukamilisha miradi mbalimbali ya maji iliyokuwa imesimama kutokana na changamoto mbalimbali.

Alisema miradi mingi ya maji ambayo ilikuwa inapata ufadhili wa fedha kutoka kwa wahisani ilikuwa imesimama kwa muda mrefu , lakini kwa sasa baada ya kuanzishwa kwa Mfuko huu fedha nyingi zimepatikana na kupelekwa kwa halmashauri za wilaya zilizokuwa zimetumiza vigezo vya hatua mbalimbali za ujenzi wake na kutumiwa fedha .

Alisema kutokana na upatikanaji wa fedha, Wizara imepanga kuona hadi kufikia Juni mwaka huu miradi yote mikubwa iliyokuwa imesimama itakamilika, hivyo kuwezesha usambazaji ,upatikanaji wa maji safi na salama kwa asilimia kubwa mijini na vijijini.