Katavi wahadharishwa juu ya ebola

MIKOA ya Rukwa na Katavi imewataka wakazi wake hususani wanaoishi katika mwambao mwa Ziwa Tanganyaka kuchukua tahadhari kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa bbola katika nchi jirani ya Jamuhuri ya Kidemorasi ya Congo(DRC).

Aidha imewatoa hofu wakazi wake kuwa ugonjwa huo bado haujaingia nchini na kwamba hakuna mgonjwa yeyote aliyehisiwa wala kuthibitishwa kuwa na virusi vya bbola . Mlipuko wa ugonjwa wa ebola nchini DRC ulitangazwa na Shirika la Afya Duniani(WHO) , Mei 12 mwaka huu , ambapo umethibitishwa kwa kupitia vipimo vya maabara baada ya kutokea wagonjwa tisa, kati yao watatu wamepoteza maisha wakati wengine sita wakiendelea na matibabu .

Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Raphael Muhuga alimewataka wakazi wa vijiji vya Ikola na Karema ambavyo viko katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika vikipakana na DRC kuchukua tahadhari ya kutosha.

“Mkoa wetu (Katavi ) hususani vijiji vya Karema na Ikola vilivyopokatika mwambao mwa Ziwa Tanganyika ambavyo vinapakana na DRC vipo hatarini kuambukizwa ugonjwa huo kutokana na mwingiliano wa watu hasa wasafiri wanaoingia na kutoka nchi hiyo jirani , hivyo tahadhari kubwa lazima ichukuliwe,” alisisitiza.

Inasemekana mlipuko wa ugonjwa huo umetokea katika Jimbo la North-East Bas Uele linalopakana na nchi ya Jamuhuri ya Afrika ya Kati (CAR) . Akifafanua alisema kuwa tahadhari iliyochukuliwa ni pamoja na kupeleka wataalamu wa afya na vifaa kinga katika vijiji vya Ikola na Karema ambavyo vina mwingiliano mkubwa wa watu wanaoingia kutoka DRC.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven aliwataka madiwani husuani wale ambao kata zao ziko katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika kushirikiana kwa karibu na maofisa uhamiaji ili kudhibiti uingiaji holela wa watu kutoka DRC.