Kiwanda cha General Tyre hakifanyi kazi, kimechakaa’

KIWANDA Cha General Tyre kilichopo mkoani Arusha hakijaanza kufanya kazi kutokana na uchakavu wa mitambo na teknolojia iliyokuwa inatumika imepitwa na wakati. Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Wete Mbarouk Salim (CUF).

Mbunge Salim alitaka kujua jitihada za serikali kufufua kiwanda hicho pamoja na kuendeleza kilimo cha mpira katika mashamba yaliyopo Tanga na Morogoro pamoja na ukubwa na umri wa mashamba hayo gani kwa umri.

Naibu Waziri Nasha alisema kiwanda hicho na mashamba ya mpira hayana uhusiano wa karibu kwani hakitumii mpira unaozalishwa kwenye mashamba hayo. “Kiwanda hicho kinatumia malighafi iliyo katika mfumo wa majora wakati teknolojia ya kugema mpira inayotumika inatoa malighafi iliyo katika mfumo wa vipande,” alisema.

Alisema mpira unaozalishwa nchini unatumika katika viwanda vingine kama vile OK plastic, Bora shoes na viwanda vingine vidogo. Vile vile, mpira huo unauzwa nje ya nchi na kuongeza kuwa zao hilo ni moja kati ya mazao ya biashara ambayo yamekuwa yakizalishwa nchini kwa muda mrefu katika mashamba yaliyopo Kalunga Mang’ula wilayani Kilombero na Kihuhwi wilayani Muheza ambayo yalianzishwa mwaka 1978.

Naibu Waziri Nacha alisema shamba la Kihuhwi lina ukubwa wa hekta 790 na shamba la Kilunga lina ukubwa wa hekta 750. “Mashamba ya mpira upande wa Zanzibar yako Mashai na Mselem Unguju yenye hekta 637.

Mashamba madogo madogo saba yaliyipo Unguja na Mpemba yana ukubwa wa hekta 633,” alisema. Ole Nasha alisema serikali inalenga kufufua kiwanda hicho na kwamba imefanya utafiti na kubani namna bora ya kukifufua na kuongeza kuwa taarifa za awali zimeeleza kuwa, mitambo iliyopo inatakiwa kubadilishwa kwa kuweka mipya inayotumia teknolojia ya kisasa