Kampuni ya uagizaji kemikali yachunguzwa

MKEMIA Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele amesema vyombo vya dola vimeanza kuichunguza kampuni ya Techno Net Scientific Ltd inayojihusisha na uingizaji na uuzaji wa kemikali nchini.

Alisema kemikali zinazoagizwa ni pamoja na bashirifu kwenye viwanda, maabara za shule, vyuo vikuu, taasisi za uchunguzi na utafiti na hospitali baada kuripotiwa inafanya kazi kinyume cha sheria.

Profesa Manyele alisema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa kutokana na taarifa hiyo, mamlaka za usimamizi ikiwa ni pamoja na maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Mamlaka ya Chakula na Dawa zilifanya ukaguzi wa pamoja.

Alisema taratibu za uchunguzi zitakapokamilika kampuni hiyo itafikishwa mahakamani. Kutokana na madai hayo, alisema serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa makampuni na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu na wanaovunja sheria katika uingizaji, usafirishaji, uhifadhi na utumiaji wa kemikali ikiwemo kemikali bashirifu nchini.

Aliwataka pia wananchi kutoa taarifa na kuwafichua wafanyabiashara ya kemikali wanaokiuka matakwa ya sheria. Kuhusu kampuni hiyo alisema wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa serikali ilitoa usajili wa muda wa miaka miwili kwa kampuni hiyo Aprili 30, 2014 usajili ambao muda wake ulikwisha Aprili 30, 2016.

“Baada ya muda huu kuisha kampuni hii iliwasilisha maombi ya kuhuisha usajili wake ambapo kwa mujibu wa sheria ya kemikali ilipaswa kusitisha shughuli zake hadi pale cheti cha usajili kitakapopatikana,” alisema.

Aliongeza kuwa hata hivyo kampuni hiyo iliendelea na shughuli za kemikali pamoja na kuwa muda wa cheti cha usajili umekwisha, pia kuna taarifa kuwa imekuwa ikiingiza kemikali nchini kwa kutumia njia za udanganyifu ikiwa ni pamoja na kutumia vibali vya bandia. Alisema kutokana na taarifa mbalimbali za kufanya kazi kinyume cha sheria, mamlaka za usimamizi zilifanya ukaguzi wa pamoja.