Safari reli ya kati sasa kuanzia Moro

UONGOZI wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), umetangaza kuhamishia kwa muda huduma ya usafiri wa treni kwenda bara katika kituo cha Morogoro kuanzia leo Jumamosi Mei 20, 2017 badala ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, shirika litalazimika kuwatafutia usafiri wa mabasi abiria waliokuwa wamekata tiketi Dar es Salaam, hivyo watasafirishwa hadi Morogoro. Uamuzi ambao umechukuliwa baada ya kipande cha reli kati ya Dar es Salaam na Ruvu kuwa hakipitiki kutokana na sehemu ya daraja la reli la Ruvu kutitia upande mmoja.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Masoko wa TRL, Shaaban Kileo alisema hayo katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam. Alisema abiria watakaohusika ni wale wenye tiketi waliokuwa waondoke jana ijumaa na wale wa kesho jumapili ambao treni zao zimefutwa.

Alisema kuhusu wafanyabiashara wasafirishaji wa shehena kwenda bara wametakiwa kuwasiliana na idara ya masoko TRL ili kupewa utaratibu wa jinsi ya kusafirisha mizigo yao hadi Morogoro ambako itasafirishwa kwa treni kwenda bara.

Alisema kutokana na hali hiyo mamlaka husika zinafanyia kazi ukarabati wa daraja hilo ili njia ya reli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ifunguliwe kwa muda mfupi iwezekanavyo.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Bodi ya TRL Profesa John Kondoro na wajumbe wengine wa bodi jana walitembelea eneo la daraja kufanya tathmini ili bodi kama mamlaka itoe maelekezo yake kuhusu maandalizi ya kazi za ukarabati wa daraja hilo.