Wabunge wataka maandamano

WABUNGE wameishauri Serikali kuunda timu ya wasomi makini, kushauriana na Kampuni ya Barrick Corporation katika kujadili urejeshaji fedha walizochota kupitia makinikia.

Aidha, baadhi yao wamesema ni vema kukafanyika maandamano nchi nzima, kumuunga mkono Rais John Magufuli, kwa kuwa jasiri na mzalendo katika kusimamia rasilimali za Taifa ikiwamo madini.

Wabunge waliyaeleza hayo jana wakati wakichangia mjadala wa Taarifa ya Hali ya Uchumi 2016 na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 iliyowasilishwa bungeni Juni 8, mwaka huu.

Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza (Chadema), aliishauri serikali kuunda timu ya wasomi makini kujadiliana na Barrick Corporation inayomiliki kampuni ya Acacia nchini, ili serikali ipate kile inachostahili.

Kampuni hiyo inaendesha migodi mitatu ya Bulyanhulu na Buzwagi mkoani Shinyanga na North Mara wilayani Tarime mkoa wa Mara. “Lazima tuchukue tahadhari kidogo. Mimi naziamini taarifa za kamati hizi mbili za Rais, tumeibiwa sana.

Lakini naishauri serikali iteue watu wasomi makini na imara ili kuhakikisha tunafanikiwa katika kile tunachokitaka,” alieleza mbunge huyo kutoka mkoani Geita. Aidha, Peneza alitaka pia mikataba yote na sheria za madini zipitiwe kwa migodi yote nchini na siyo Acacia pekee, kwani kuna wizi mkubwa unaofanyika migodini.

Mbunge huyo pia alipendekeza kuwa badala ya kuwa na tozo ya huduma ya asilimia 0.03 inayolipwa kwa halmashauri zenye migodi, uanzishwe mfuko wa maendeleo ambao kodi na tozo zake zijenge miradi ya maendeleo kwa jamii husika zinazungukwa na migodi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Mayenga (CCM), pia alipendekeza kuundwa kwa timu imara ya washauri kwa upande wa Tanzania. “Mimi nimekuwa katika Bodi ya Williamson Diamond kwa miaka minane. Najua biashara hii (ya madini).

Ushauri wangu ni kwamba tunapokwenda kuzungumza nao tuwe na watu makini. “Wenzetu hawa ni wazuri katika upembuzi, katika biashara na wana uzoefu, na ni ma-tycoons katika maeneo mbalimbali duniani,” alieleza Mayenga anayetoka mkoani Shinyanga, ambako kuna migodi mbalimbali ya madini.

Mbali ya kumtaja Rais Magufuli kuwa amefanya kazi kama ya miaka saba wakati ndio kwanza ana miaka miwili madarakani, alisema Rais amekuwa mstari wa mbele katika kusaidia wananchi wanyonge wa Tanzania.

Aidha, aliitaka Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kubadili uamuzi wa kuruhusu kampuni za madini kuweka fedha zao katika benki za nje. Pia aliishambulia Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali akisema kuwa imeoza na inashiriki katika kuruhusu kemikali za hatari kuingizwa nchini bila kufuata taratibu.

Naye Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige (CCM), alikuwa na ushauri kwa serikali kuhusu muafaka na Barrick. Maige alipendekeza kuwa katika majadiliano hayo, halmashauri yao ya Msalala ilipwe kwanza fedha zake Sh bilioni 795 kama ilivyotajwa katika Kamati ya Profesa Nehemia Osoro ya wachumi na wanasheria.

Pia kuboreshwa kwa mikataba hasa katika kampuni zinazotoa huduma, pia Barrick walipe fedha za kusaidia jamii kiasi cha Sh trilioni 1.3, fidia kwa wafanyakazi na watu zaidi ya 4,000 waliotwaliwa ardhi yao, kufanyika uchunguzi katika migodi mingine na kinu cha uchenjuaji kijengwe Kahama kwa sababu kuna migodi mingi.

Maige pia alisema wataomba kibali wilayani Kahama ili kuandamana kumuunga mkono Rais Magufuli. Suala la maandamano pia liligusiwa na Mbunge wa Hanang, Dk Mary Nagu (CCM), aliyesema kuwa Taifa zima linapaswa kurindima kwa maandamano, kuonesha mshikamano wao na Rais Magufuli.

“Hili la madini tulishughulikie sote, na ingefaa tungekuwa na maandamano nchi nzima kumuunga mkono Rais kwa ujasiri wake. Nchi ingerindima kwa maandamano kuonesha mshikamano,” alisema Dk Nagu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kiteto, Emmanuel Papian (CCM), alipendekeza kuwa kabla ya kuanza majadiliano, Barrick walipe Sh trilioni 35 ikiwa ni ahadi ya kwamba watalipa fedha walizochota kwa takriban miaka 20.

Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema suala la makinikia ni la kuungwa mkono na Watanzania wote, na kushauri mikataba na sheria za madini zipelekwe bungeni kufanyiwa marekebisho haraka.

Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omar Mgumba (CCM), alisema maneno ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwamba anawaachia Watanzania chuma, yametimia. “Rais Kikwete alisema yeye anaondoka na anatuachia chuma kinachotema cheche, ni kweli cheche sasa tunaziona.

Tofauti na marais waliopita, huyu ni mpole kidogo. Ni vyema akaongeza ukali,” alisema Mgumba. Wabunge hao na wengine waliochangia mjadala huo wa Bajeti ya Serikali, walisisitiza haja ya fedha za tozo za mafuta kupelekwa kwa ajili ya kusaidia maji vijijini