Afungwa maisha kwa kumlawiti mpwawe

Mkazi wa Kata ya Kimagai Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Peter Semango (23) amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani baada ya kukiri kumlawiti mtoto wa dada yake mwenye umri wa miaka minane.

Mtu huyo amedai mahakamani  kuwa alifanya hivyo, kutokana na kuzidiwa na hisia za mapenzi. Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Pascal Mayumba alitoa adhabu hiyo baada ya mshitakiwa kukiri shitaka hilo.

Awali, Hakimu Mayumba alipomuuliza mtuhumiwa kuhusu tuhuma hizo, alikiri kufanya makosa hayo, akidai kuwa alikuwa amezidiwa na hisia za mapenzi baada ya kukaa muda mrefu bila kufanya kitendo hicho.

Ilielezwa kuwa siku ya tukio, mshitakiwa alifanya kitendo hicho, akitambua kuwa anayemfanyia ukatili huo ni mtoto mdogo, tena mtoto wa mdogo wake wa damu. Akijitetea, kabla ya hukumu hiyo kutolewa, mshitakiwa aliomba Mahakama impunguzie adhabu, akisema umri wake ni mdogo na hana ndoa.

Awali, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Godwill Ikema aliiambia Mahakama kuwa mshitakiwa anakabiliwa na makosa matatu ya kubaka, kulawiti na kufanya mapenzi na mahalimu (ndugu wa damu yake).

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Juni 13 mwaka huu katika Kijiji cha Kimagai majira ya saa nne usiku, alimlawiti mtoto wa dada yake mwenye umri wa miaka minane (jina linahifadhiwa).