Maaskofu: Mungu amejibu maombi

BARAZA Kuu la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) limetoa tamko la kumpongeza Rais, Dk John Magufuli kutokana na kupigania rasilimali za nchi ambazo ziliumbwa na Mungu.

“Kama Maaskofu tukasema tusikae kimya lazima tuseme kitu kwa ajili ya shujaa na jemedari huyo anayesemea Watanzania. Mungu ametupatia mtu wa muhimu sana,” lilisema sehemu ya tamko hilo.

Katika tamko lao lililosomwa juzi na Askofu Peter Konki mbele ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, limesema hakika Tanzania imepata kiongozi kutokana na maombi mazito yaliyofanywa na viongozi wa dini na waumini na sasa rasilimali za nchi zinakwenda kukombolewa ili ziwanufaishe Watanzania wote.

Akisoma, Askofu Konki alisema baraza lilipokaa liliona si busara kukaa kimya kutokana na kuwa na tukio kubwa hapa nchini na kuamua kutoa tamko la kumpongeza Rais Magufuli juu ya uponyaji wa maliasili za nchi ambazo zimeumbwa na Mungu.

“Rais Magufuli kwa muda mfupi aliokaa madarakani amefanya mambo mengi, Rais ni mvumilivu na anajua cha kufanya ameleta mageuzi makubwa nchini amewaona wenye vyeti feki na watumishi hewa na kuwaondoa kwenye utumishi wa umma,” alisema.

Pia alisema katika suala la madini, Rais amefanya kazi kubwa na kugundua rasilimali ya nchi ilivyokuwa ikitoroshwa huku ikiwaacha Watanzania wakiwa masikini. Alisema Rais Magufuli ni kiongozi shujaa ambaye anatakiwa kupongezwa kutokana na kazi kubwa anayofanya.

“Serikali ijue Wapentekoste wana dhamira na serikali na wako nyuma ya Serikali, tunajua Rais anajeruhiwa na maneno mengi Sisi CPCT siku zote tunaunga mkono Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tunaona juhudi katika utendaji kazi,” alisema.

Askofu Konki alisema katika kikao cha kawaida walichokaa Mjini Dodoma walijadili juhudi za Serikali na wamejionea jinsi serikali ya awamu ya tano tangu iingie madarakani imejitanabaisha katika kupambanua na matendo ya kifisadi na hayo ni majibu ya kanisa kutoka kwa Mungu.

“Uongozi uliotukuka, hali ya utukufu na amani ni zawadi kutoka kwa Mungu na tunamrudishia sifa na shukrani kwa kutuonesha ni kwa namna gani madini yetu yalikuwa yakiporwa,” alisema.

Alisema kama maaskofu wanamuahidi Rais Magufuli kuendelea kumuombea na kumuunga mkono kama jemedari wa taifa na aendelee na kazi ya kunyoosha nchi kwani ameweza kudhibiti matumizi ya serikali na kuongeza juhudi katika ukusanyaji kodi.

Alisema kama kanisa wataendelea kumuombea Rais Magufuli, Mungu ampe afya njema, hekima na busara wakati anatekeleza majukumu yake. “Tunawaombea na viongozi wa nchi Mungu awape hekima, busara na uaminifu bila kuathiriwa na matamanio ya muda mfupi yatokanayo na maslahi ya kisiasa,” alisema.

Naye Mwigulu Nchemba alisema uchaguzi wa mwaka 2015 ni uchaguzi ulioombewa sana na walikuwa wakiomba Mungu awape Rais mwenye roho ya pekee na kazi alizofanya zimekuwa na utukufu.

“Kwenye uchaguzi uliopita kama si maombi nchi hii ingebadilika lakini wacha Mungu kwa maombi yao uchaguzi ukapita salama. Mungu alisikia mambo na akajibu sawa sawa na mapenzi yake tuendelee kumuombea Rais Magufuli afanye kazi yake ili sifa na utukufu vimrudie Mungu,” alisema.

Alisema kama kiongozi anaiona nia njema aliyonayo Rais kwa Watanzania. “Tumuombee Rais wengine wanasema mbona Rais anakuwa mkali ni lini uovu ukaondoka kwa upole, mnatambua mapepo yapo halafu unasema shetani toka basi, huwezi kubembeleza pepo hata siku moja,” alisema.

Alisema hata Yesu kwa mambo ya kibinadamu alipoona pepo akasema kwa ukali shetani toka. Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige alisema alisema tamko la kumpongeza Rais ni zuri kwani anastahili kupongezwa kutokana na kazi kubwa anayofanya.

“Ufisadi uliogundulika ni kiasi kidogo sana lazima tuambiwe vile vitofali vya dhahabu vilizalishwa vingapi na vina thamani gani hapa tunazungumzia mchanga tufike na kule kwenye vitofali,” alisema.