Wasomi wawashambulia wenzao vigeugeu

WASOMI wa vyuo vikuu nchini wameibuka na kuwashambulia wasomi wenzao, waliopewa dhamana kutumikia Serikali, wakisema wamekuwa vigeugeu dhidi ya Watanzania huku wengine wakitumia usomi wao kujineemesha wenyewe.

Baada ya kupokea Ripoti ya Kamati ya Pili ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusu mchanga wa madini unaosafirishwa nje ya nchi, Rais John Magufuli alisema inashangaza hata wasomi walioaminiwa, walishindwa kutumia dhamana waliyopewa na badala yake, wakawa sehemu ya kulisaliti taifa.

Miongoni mwa wanaotuhumiwa kutumia usomi wao vibaya na kulitumbukiza taifa katika hasara ya takribani shilingi trilioni 108, ni pamoja na waliokuwa watumishi wa nyadhifa tofauti, hususan mawaziri wa nishati na madini tangu mwaka 1998 hadi mwaka 2017, pamoja na wanasheria wakuu wa serikali.

Rais alitoa mfano wa wasomi wenye shahada ya uzamivu 17 waliopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lakini wakashindwa, kutumia usomi na uzalendo wao kufuatilia na kujua namna rasilimali za Tanzania zinavyotoroshwa kupitia mauzo ya makinikia na dhahabu.

Pamoja na kumpongeza Rais John Magufuli kwa kusimamia kikamilifu rasilimali za taifa na kuwataka wasomi wenzao kuacha kuwa vigeugeu, waliwataka wasomi na Watanzania kwa jumla kusimama pamoja kama taifa, kwa kuwa fedha na rasilimali za nchi hufaidisha wote bila kujali vyama vyao.

Pongezi na mwito huo vilitolewa kwa nyakati tofauti jana Dar es Salaam, kwenye Kongamano la Mtazamo wa Wasomi wa Vyuo Vikuu kuhusu ripoti za mchanga wa madini zilizowasilishwa kwa rais na tume maalum mbili zilizokuwa na kazi tofauti.

Wakichangia katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (TAHLISO), Stanslaus Peter alisema Rais Magufuli anapaswa kupongezwa kwa hatua aliyoichukua na kusema ni kiongozi anayefuata nyayo za Mwalimu Julius Nyerere.

“Kama wasomi tumeona ni vyema tunajadili taarifa ya madini zilizowasilishwa mbele ya rais ambazo wote tumesikia jinsi rasilimali zetu zilivyoibiwa, rais anapaswa kupongezwa, amekuwa mzalendo kwenye hili na kulisimamia kidete, huyu ni rais anayefuata nyayo za Nyerere,” alisema Peter.

Aidha, aliwataka wasomi wenzao kuacha kuwa vigeugeu na badala yake wasimame pamoja kama taifa, kumuunga mkono rais kwa sababu fedha zitakazopatikana kwenye rasilimali hiyo zitanufaisha wote bila kujali itikadi za vyama vyao.

Akichangia kwenye kongamano hilo, Kilango Benjamin kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, alisema uzalendo wa Rais Magufuli, ndio umefichua hayo yote yaliyobainika kwenye ripoti hizo mbili kuhusu madini ya taifa.

“Ni uzalendo wa rais wetu ndio umeibua haya yote, vinginevyo tungeendelea kuibiwa kwa kuwa hata viongozi walioaminiwa hawakuwa wazalendo,” alisema Benjamin. Hivyo akasisitiza ipo haja sasa kwa serikali kuangalia upya mtaala wa elimu unaotolewa nchini ili kuingiza somo la uzalendo kuanzia ngazi ya elimu ya msingi kwa lengo la kuwajenga Watanzania na kuwafundisha jinsi ya kuwa wazalendo kwa nchi yao.

Kwa upande wake, Felix Bahati msomi kutoka Chuo Kikuu cha St John pamoja na kumpongeza rais kwa uthubutu wake na uzalendo, aliomba serikali kuvunja mikataba ya madini kwa kuwa haina faida kwa taifa.

“Ni vyema serikali ikavunja mikataba ya madini tumeona haina maslahi kwa taifa, na badala yake mingi inanufaisha wawekezaji, tuanze upya na kuangalia pia sheria zetu ili ziwe na tija kwa maslahi ya taifa,” alisema Bahati.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Mombeki Kaiza alisema ipo haja kwa rais kuangalia upya jinsi ya kupunguza madaraka aliyopewa Waziri wa Nishati na Madini ambayo kwa mujibu wa sheria ya madini ya sasa, ndiye mwenye dhamana ya kuingia mikataba mbalimbali ya rasilimali hiyo.

Akizungumzia Sera za madini, msomi kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Alex Stephano alisema tatizo kwenye sekta ya madini sio ubovu wa sera bali ni utekelezaji wake na aina ya watumishi waliopewa nyadhifa kusimamia maeneo hayo.

“Tuna sera nzuri za madini ila tatizo ni aina ya viongozi tuliowapa eneo hilo kulisimamia, hawana uzalendo na ndiyo chanzo cha matatizo haya yote leo, lazima sasa tubadilike na kufunzwa uzalendo ili tuweze kuwa na uchungu wa rasilimali za taifa letu,” alisema Stephano.

Awali alichokoza mada kuhudu Sera za madini kama zina manufaa kwa taifa, Msomi wa masuala ya Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Willium Haule alisema sera ya madini ni nzuri na ni moja ya sera bora barani Afrika, lakini tatizo ni utafsirishwaji wake.

“Tuna sera nzuri ya madini, sera yetu ni moja ya sera nzuri barani Afrika, lakini tatizo linakuja kwenye kutafsiriwa na pia kwenye usimamizi wa sera yenyewe,” alisema Haule. Akifafanua kidogo kuhusu sera, Haule alisema sera ni muongozo wa kufikia malengo na kwa kila sera zipo za aina tofauti kulingana na aina ya utawala na falsafa.

Kuhusu sera ya madini alibainisha zipo aina mbili za falsafa, moja ni ile rasilimali ya utaifa na pili ni ile inayolenga rasilimali ya kibepari. Alisema kwa hali ilivyo, madini ya Tanzania yalikuwa yakielemea kwenye sera ya falsafa ya rasilimali ya kibepari ambayo wawekezaji walikuwa na mamlaka zaidi kuliko mmiliki wa rasilimali yenyewe na kwamba Rais Magufuli alichofanya ni kurudisha rasilimali hiyo kuwa falsafa ya taifa.

Naye Msomi wa Sheria kutoka (UDSM), Hamza Jabir alihoji marekebisho yote ya sheria za madini yaliyowahi kufanya hapo awali yalikuwa na tija kwa taifa? Na je nchi ina wataalamu wa sheria wabobezi wanaoweza kufanya majadiliano na wawekezaji hao.

Kongamano hilo limekuja ikiwa ni siku sita zimepita tangu Rais Magufuli akabidhiwe ripoti ya pili ya timu ya wataalamu iliyoundwa kuchunguza hasara za kiuchumi na kisheria kuhusu mchanga wa madini tangu nchi ilipoanza biashara ya kusafirisha mchanga huo nje ya nchi yapata miaka 19 sasa.

Katika ripoti hiyo ilibainika kuwa taifa hupoteza zaidi ya Shilingi trilioni 108 katika kipindi cha miaka hiyo, kuanzia mwaka 1998 hadi Machi mwaka huu. Baada ya ripoti hiyo kutoka, Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ndio mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Miningi Limited, Profesa John Thornton aliwasili nchini Juni 14 na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli.