Samia azindua rasmi soko la ajira China

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewataka wahitimu wa vyuo vikuu nchini, kujitofautisha na wengine katika soko la kupata ajira kwa kufanya bidii pamoja na kuwa washindani.

Samia alisema hayo jana alipokuwa akizindua fursa za ajira kwa Watanzania ambazo zinatolewa na kampuni 120 kutoka China na chache za kizalendo za hapa nchini eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema kwa vijana ambao bado wapo vyuoni inawabidi wasome kwa bidii ili fursa kama hiyo itakapotokea tena wawe wamejiandaa vema. “Naunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya China kwa kupitia taasisi ya Confucius iliyopo chuoni hapa kwa kushirikiana na Tanzania za kutoa fursa za ajira kwa vijana wa vyuo vikuu nchini waliohitimu.

“Pia kwa nyie wahitimu mnatakiwa mjitofautishe na wengine katika soko na kufanya kwa bidii kwenye soko la dunia,” alisema. Awali, Balozi wa China nchini, Dk. Lu Youging alisema kampuni zaidi ya 100 kutoka China zitatoa ajira kwa vijana waliohitimu vyuo vikuu kwa lengo la kuisaidia serikali ya Tanzania, kwani hilo ni jambo kubwa kwa kuwa vijana ni taifa la kesho.

Alisema Serikali ya Tanzania imeweka uzito kwenye maendeleo ya vijana kwa kutoa fedha nyingi ili wapate fursa ya kusoma ili baadaye wapate ajira ambayo itaboresha maisha yao.

Alisema kutokana na urafiki uliopo baina ya China na Tanzania ndio maana wameshiriki katika kutoa nafasi hizo za ajira kwa vijana wa Kitanzania Alisema hivi sasa uwekezaji wa China nchini Tanzania ni dola za Kimarekani bilioni 7 (Sh trilioni 14.7), ambapo zaidi ya kampuni 100 zinazofanya kazi nchini zimetoa ajira zaidi ya Watanzania 1,200.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala alisema siku ya jana ilikuwa ni maalumu kwa chuo hicho na Tanzania kwa kuwa wenyeji wa tukio hilo kubwa la vijana kutafuta ajira katika kampuni kutoka China.

Alisema kwa tukio hilo anaamini idadi kubwa ya vijana watapata nafasi ya kufanya kazi na watu wa China, hali inayoonesha moyo wa kweli uliomo baina ya urafiki wa nchi hizo mbili.

Pia aliwaasa vijana watakaobahatika kupata nafasi hiyo kujifunza kwa bidii kutoka kwa wafanyakazi wenzao na viongozi watakaowaongoza, kuongeza ujuzi na maarifa, pia kuendeleza utamaduni na mahusiano.