Sakata la makinikia latawala mjadala wa bajeti

BAJETI ya Serikali kwa Mwaka 2017/18 mjadala wake unahitimishwa kesho huku sakata la makinikia likichukua nafasi kubwa. Siku ambayo mjadala huo ulianza Juni 12, mwaka huu ndio siku ambayo Rais John Magufuli alipokea ripoti ya kamati yake ya pili ya uchunguzi kuhusu mchanga wa dhahabu (makinikia).

Tangu siku hiyo, wabunge wote wale wa CCM na Upinzani, wakajikuta katika mjadala mzito kuhusu yale yaliyoibuliwa na Kamati iliyoongozwa na Profesa Nehemia Osoro. Pongezi nyingi zikaelekezwa kwa Rais Magufuli kwa kuunda kamati hiyo na ile ya wanasayansi iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma, ambazo zote zilikuja na matokeo yaliyoonesha wizi mkubwa katika sekta ya madini.

Wabunge waliochangia Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa Juni 8, mwaka huu wakajikuta hawana budi kusema kitu kuhusu madini. Miongoni mwa michango ya wabunge katika madini ni pongezi kwa Rais Magufuli na kutaka umma wa Watanzania umuunge mkono. Katika kudhihirisha kuwa Bunge nalo limeguswa na kazi nzuri ya Dk Magufuli lilipitisha Azimio katikati ya mjadala wa bajeti, kumpongeza rais kwa kazi ya ujasiri na uzalendo ya kulinda rasilimali za umma.

Katika Azimio hilo lililowasilishwa na Mbunge wa Newala Mjini, George Mkuchika, wabunge walimpongeza Rais na kuahidi kuwa Bunge liko bega kwa bega naye na litampa ushirikiano katika kazi ya kulinda rasilimali za Taifa. Wabunge wawili, Ezekiel Maige wa Msalala na Dk Mary Nagu wa Hanang, walienda mbali zaidi na kutaka kufanyika maandamano nchi nzima kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri.

Mbali na hilo, wabunge walisimama kwa dakika moja kumpa heshima Rais Magufuli (standing ovation) kutokana na ujasiri wake na uzalendo kwa Taifa. Ukiacha pongezi kwa Dk Magufuli, mchango mwingine wa wabunge katika sakata la makinikia ni kutaka kuletwa haraka kwa mikataba na sheria zote za madini ili zifanyiwe marekebisho haraka kwa nia ya kuziba mianya ya wizi. Wabunge wote waliochangia, walieleza kuwa sheria na mikataba mibovu ya madini ni chanzo cha wizi na upotevu mkubwa wa mapato kupitia makinikia na madini mengine nchini.

Ingawa wabunge wa Upunzani walielekeza lawama kwa wenzao wa CCM kwa madai ya kushiriki kupitisha mikataba na sheria mbovu, walipongeza hatua alizochukua Rais Magufuli. Lakini pia baadhi yao, walitaka kuchukuliwa hatua kali kwa wote waliotajwa katika sakata la makinikia. Miongoni mwa waliotajwa ni mawaziri wa zamani wa nishati, makamishna wa madini na wanasheria wakuu wa zamani. Wabunge watatu Dk Dalaly Kafumu, Andrew Chenge na William Ngeleja ni miongoni mwa waliotajwa katika sakata hilo, ambalo baada ya ripoti ya Profesa Osoro, nchi nzima mjadala ni huo.

Hata hivyo, Ngeleja akichangia Bajeti mwishoni mwa wiki licha ya kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri, alisema kutuhumiwa sio kupatikana na hatia. Waziri huyo wa zamani wa Nishati na Madini alisema “tunachapa kazi na tunasonga mbele.” Ukiondoa sakata la makinikia, mjadala wa Bajeti unaohitimishwa kesho kwa kura ya wazi kwa kila mbunge, haukuwa mzito sana zaidi ya wabunge wengi kuisifu bajeti hiyo ya Sh trilioni 31.7.

Wabunge walipongeza hatua zilizochukuliwa na serikali katika kuondoa tozo na kodi zilizokuwa kero kubwa kwa wananchi. Kuondolewa ushuru au kupunguzwa katika mazao, vyakula vya mifugo, magari, vifaa vya walemavu, ni miongoni mwa mambo yaliyowagusa watunga sheria hao wa Tanzania. Kesho Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango atakuwa na kazi nyepesi ya kujibu hoja kinzani chache tu. Atahitajika kujibu hoja kuhusu tozo ya mafuta iliyoongezwa kwa Sh 40, ambayo wabunge wote walitaka ipelekwe katika Mfuko wa Maji Vijijini.