Mimba zakatisha masomo kwa wanafunzi 2,800

WASICHANA 2,892 waliokuwa wanafunzi wa shule za msingi na 22 wa sekondari katika wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa, wamekatisha masomo kutokana na kupata mimba na ndoa za utotoni.

Sababu nyingine zilizotajwa kusababisha wasimalize masomo yao ya msingi na sekondari ni utoro. Hayo yalibainishwa na Ofisa Maendeleo ya Jamii, wilayani Nkasi, Mary Siame wakati akifunga sherehe za maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofadhiliwa na kuratibiwa na Shirika la Plan International Tanzania ambayo yalihudhuriwa na wanafunzi, walimu wao na watoto kutoka kata za Mtenga, Mkwamba na Nkandasi.

Shirika hilo ambalo limepata ufadhili wa mradi wa kuzuia ndoa za utotoni kutoka Shirika la Norway Agency for Development (Norad), kuwezesha kuhamasisha jamii kuhusu athari za ndoa za utotoni. Mradi huo unatekelezwa wilayani Kilombero, mkoa wa Morogoro na Nkasi, mkoani Rukwa kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2019.

Siame alisema mimba za utotoni na wasichana kushindwa kumaliza elimu ya msingi ni tatizo lililokithiri katika wilaya hiyo ambapo watoto wa kike walioandikishwa kuanza darasa la kwanza mwaka jana walikuwa 4,917, watoto wa kike 2,871 hawakumaliza elimu ya msingi kwa sababu kadhaa ikiwemo mimba na ndoa za utotoni.

Alisema takwimu hizo ni hadi Juni mwaka huu. Alisema upande wa shule za sekondari wasichana 22 walipata ujauzito huku 20 wakiwa ni watoro sugu. Akizungumza na gazeti hili kando ya sherehe hizo, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Chala iliyopo wilayani humo alisema kuwa wanafunzi 10 waliokuwa wakisoma katika shule hiyo wamekatisha masomo baada ya kupata ujauzito na kuolewa katika kipindi cha mwaka mmoja.

“Baadhi ya wanafunzi waliokatiza masomo yao baada ya kupata ujauzito ni wale wanaoishi mbali na shule, wapo wanaolazimika kutembea zaidi ya kilomita 20 kila siku ili kuhudhuria masomo hapa shuleni,” alisema. Alisema kuwa wanafunzi hao wanaishi katika vijiji vya Mbwendi mashambani ambacho ni umbali wa kilomita 10 kutoka shuleni.

Meneja wa Shirika la Plan International wilayani Nkasi, William Mtukananje alisema shirika hilo linatekeleza miradi mikubwa miwili ukiwemo wa kuzuia ndoa za utotoni ambao utatekelezwa katika kata tatu za Mtenga, Mkwamba na Nkandasi na mradi wa afya ya mama na mtoto unaotekelezwa mkoani Rukwa.