Kigoma kuongeza uzalishaji wa kahawa kwa wingi

MKOA Kigoma uko kwenye mkakati kabambe wa kuongeza uzalishaji wa kahawa ili kuufanya mkoa huo kuwa moja ya mikoa inayozalisha kahawa kwa wingi, kukidhi mahitaji ya ongezeko la kahawa kwenye soko la dunia.

Meneja wa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa(TaCRI), Epimaki Tarimo amesema hayo wakati wa mkutano mkuu wa chama kikuu cha wakulima wa kahawa mkoa Kigoma (Kanyovu) na kusema kuwa mkoa huo unazalisha kiwango cha chini cha kahawa kwa sasa.

Katika hilo alisema utekelezaji wa mpango huo umejikita katika kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kwa kutumia kituo chake cha uzalishaji mbegu kilichopo kwenye kijiji cha Mwayaya wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.

Pamoja na kuzalisha mbegu hizo ambazo zinastahimili magonjwa, pia taasisi yake imejipanga kuhakikisha mbegu hizo zinasambazwa kwa wakulima na zinatumiwa sambamba na kuhimiza matumizi ya mbolea hasa samaki katika kurutubisha ardhi. Akizungumza katika mkutano huo Meneja Mkuu wa Kanyovu, Jeremia Nkangaza ameitaka serikali kutoa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa kahawa ili kuwezesha wakulima kutumia pembejeo hizo katika kuongeza uzalishaji na kuongeza ubora wa mazao yao.

Pamoja na hilo, Meneja huyo Mkuu wa Kanyovu ameitaka serikali kupitia bodi ya kahawa kusimamia kwa karibu mpango wa kupiga marufuku ununuzi wa kahawa kienyeji, unaofanywa na wafanyabiashara binafsi ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa ubora.

Naye Mwenyekiti wa Kanyovu, Rashidi Ally alisema kuwa utayarishaji wa kahawa kienyeji bila kufuata misingi 12 ya kilimo cha kahawa ni moja ya chanzo cha kushusha ubora wa kahawa inayozalishwa mkoani Kigoma.