Ma-Dj wasaidia kudhibiti ajali Mara

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani katika Mkoa wa Mara, limesema mafanikio katika kudhibiti ajali za barabarani yanatokana na mchango wa wadau mbalimbali wakiwamo washereheshaji (MC) na wapiga muziki (Ma-Dj).

Akizungumza na HabariLeo, Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa wa Mara, Mrakibu wa Polisi (SP), Michael Deleli, alisema miongoni mwa mbinu wanazotumia kudhibiti ajali barabarani ni pamoja na kutoa elimu na kuwashirikisha wadau mbalimbali huku wakizingatia usimamizi makini wa sheria.

Alisema kufanikisha hilo, Polisi mkoani Mara wamewahimiza MC na Dj kuhakikisha kila mikusanyiko wanayotoa huduma zikiwamo sherehe za harusi na nyingine, wanapiga nyimbo zenye maudhui ya kulinda usalama barabarani kuepusha ajali.

“Tumewapa nyimbo zinazohimiza kutii sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuwakumbusha wageni katika sherehe wanazohudumia. Hili nalo limesaidia sana maana wakiwa ukumbini wanakunywa vinywaji mbalimbali, wanakumbushwa wakitoka wazingatie udereva makini na usalama barabarani,” alisema Deleli.

Aliongeza, “Kwa kweli hapa hatuna mchezo. Tumedhibiti sana, hata hawa bodaboda ambao katika sherehe mbalimbali yakiwamo maandamano hupata mihemuko na kuvunja sheria za usalama barabarani; hapa hawana mchezo huo. Akikamatwa ni moja kwa moja mahakamani.