Mrithi wa Mghwira ACT aanza na ziara

KAIMU Mwenyekiti wa Chama cha ACTWazalendo, Yeremia Maganja, anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi katika mikoa saba ya Tanzania Bara, kukagua uhai wa chama na maandalizi ya uchaguzi wa ndani ya chama, ambao upo katika ngazi ya mitaa kwa sasa.

Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho kwa vyombo vya habari, ziara ya Maganja itaanzia mkoani Mara Jumatatu ijayo. Anatarajiwa kufuatana na Katibu wa Kamati ya Kampeni na Uchaguzi, Mohamed Massaga.

Watazuru pia mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Manyara, Arusha na Kilimanjaro. Baada ya ziara hiyo itakayomalizia Julai 25, Maganja atafanya tathmini ya kina na kutembelea mikoa mingine kujitambulisha. Maganja ameshika nafasi hiyo baada ya Mwenyekiti wake, Anna Mghwira kuteuliwa na Rais, Dk John Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.