Maeneo 6 yatafutwa dhahabu

SERIKALI kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kupitia Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) imeanza kufanya utafiti wa kijiosayansi unaohusisha uchorongaji wa miamba ili kubaini maeneo yenye dhahabu katika maeneo sita nchini.

Utafiti huo umeanza ikiwa ni miezi mitano ipite tangu wachimbaji wadogo kufariki dunia kutokana na kuangukiwa na kifusi katika mgodi wa Buhemba, wilayani Butiama.

Akizungumza jana katika eneo la Biatika wilayani Butiama ambako mashine za kubaini maeneo yenye madini zinafanya uchorongaji, Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji kutoka Stamico, Alex Rutagwelela, alisema serikali imeamua kusaidia wachimbaji wadogowadogo wa madini nchini ili kuwarahisishia kujua ni maeneo gani yenye madini, wasiwe wanachimba kwa kubahatisha kama walivyokuwa wakifanya hapo awali.

Alisema mradi huo wa kubaini maeneo sita ambayo baada ya kubaini yataanzishwa vituo vya mfano vya utafiti umefadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), kupitia wizara ya nishati na madini na utagharimu dola za kimarekani milioni 3.7 (Sh bilioni 8.2).

Aliyataja maeneo yaliyopendekezwa kuanzishwa vituo vya utafiti kuwa ni kituo cha Itumbi, Chunga (Mbeya), Katente huko Ushirombo (Geita), Buhemba, Butiama (Mara), Mpanda (Katavi), Kange (Tanga), Kyerwa (Kagera) na Masakasa mkoani Lindi ambapo Mara.

Alisema jumla ya meta 1,500 za uchorongaji wa aina ya dhahabu zinatarajiwa kuchorongwa ili kupata sampuli zitakazopelekwa maabara kwa ajili ya utambuzi wa mashapo yaliyopo katika eneo hilo.

Mashine hizo zina uwezo wa kwenda chini hadi meta 2,000 na kutambua kiasi cha madini kilichopo na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo mwezi ujao. Alisema watachimba mashimo 15 hadi 18 kwa ajili ya utafiti katika wilaya ya Butiama ambapo awali wachimbaji wengi wao walikuwa wanafika meta 50 tena kwa kutumia zana duni.

Naye Machela Maseke, mchimbaji mdogo aliishukuru serikali kwa kuwaletea watafiti na wataalamu ambao wanawasaidia kubaini maeneo yenye dhahabu, hivyo kusaidia kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha