Wasichana waburuza wavulana matokeo kidato cha sita

Matokeo ya kidato cha sita yametolewa leo Jumamosi na kuonyesha kuwa wasichana wameongoza kwa ufaulu ambapo kati ya wasichana 28,731 waliofanya mtihani, waliofaulu ni ni 27,577 (97%).

Wavulana, waliofaulu ni 42,975 (95%) kati ya 46,385. Jumla ya watahiniwa 75, 116, walifanya mtihani mwezi Mei mwaka huu. Taarifa iliyotolewa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), inaonyesha kuwa watahiniwa 58,556 (93%) walipata daraja la kwanza hadi la tatu.

Kati ya hao, wasichana ni 22, 909 na wavulana ni 35,647. “Mchanganuo wa ufaulu katika madaraja unaonyesha kuwa watahiniwa walipata daraja la I na II umepanda kwa asilimia 0.59 kutoka asilimia 93.13 mwaka 2016 hadi 93.72 mwaka huu,” imesema taarifa hiyo.

Ufaulu katika madaraja kwa upande wa wasichana umepanda ikilinganishwa na wavulana. Ubora wa ufaulu kwa wasichana ni asilimia 94.07 ikilinganishwa na asilimia 93.49 ya wavulana.

Taarifa hiyo imeonyesha kuwa ufaulu kwa watahiniwa wa shule kwa upande wa masomo, ya Sayansi, Biashara, Lugha na Sanaa, haukuonyesha tofauti kubwa ukilinganisha na mwaka jana. Hata hivyo, ufaulu katika somo la General Studies umeshuka kwa asilimia 7.54 kutoka asilimia 71. 24 mwaka jana hadi 63.70 mwaka huu.

Shule kumi bora kitaifa ni Feza Girls (Dar), Marian Boys (Pwani), Kisimiri (Arusha), Ahmes (Pwani), Marian Girls (Pwani), Mzumbe (Moro), ST. Marry Mazinde Juu (Tanga), Tabora Boys (Tabora), Feza Boys (Dar) na Kibaha (Pwani).