Lukuvi akesha ofisini akitatua kero za ardhi

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, usiku wa kuamkia jana alitumia takribani saa 20 kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa tisa usiku kusikiliza wananchi 189 wenye matatizo ya kero za ardhi ofi sini kwake.

Hayo yamethibitishwa na Ofisa Habari wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Hassan Mabuye. Alisema waziri Lukuvi alifanya hivyo baada ya wananchi wenye kero, kugoma kutoka ofisini kwake, wakitaka hadi kero zao zisikilizwe.

Baadhi walilazimika kulala wizarani hapo, wakisubiri kuonana na waziri kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya wananchi hao. “Wananchi wengi wenye matatizo na kero za ardhi kutoka maeneo ya Bagamoyo, Kibaha, Mkuranga, Kibiti na Dar es Salaam kwa ujumla wametumia fursa hii ya kipekee ya kuonana na waziri mwenye dhamana ya ardhi na kumuelezea kero zao na hatimaye kupatiwa ufumbuzi papo hapo,” alisema Mabuye.

Aliongeza kuwa wananchi hao wamesifu hatua ya Lukuvi, kukutana nao ana kwa ana na kuzitatua kero zao za ardhi, huku akisema haijawahi kutokea. Mmoja wa wananchi hao, Francis Kamara, mkazi wa Ilala, Dar es Salaam alimuomba waziri huyo awawajibishe watumishi wanaokwamisha jitihada zake, kiasi cha kumfanya atumie muda mwingi ofisini kurekebisha makosa ya watendaji wake.

Mwanzoni mwa Juni 2017, Waziri Lukuvi alitoa tangazo la kuwataka wakazi wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, ambao wangependa kumuona, wafike katika ofisi yake ya Kanda ya Dar es Salaam iliyopo ghorofa ya pili, jengo la Wizara ya Ardhi – Magogoni, Kivukoni ili kujiandikisha majina yao, anuani na namba zao za simu.

Lukuvi ameahidi kufanya ziara katika kanda nyingine ili kuendelea na kazi ya kutatua migogoro ya ardhi, aliyoianza katika Kanda ya Dar es Salaam na Pwani.