Mahujaji 2500 kwenda Hijja

MAHUJAJI zaidi ya 2,500 wa Tanzania wanatarajiwa kwenda kushiriki ibada ya Hijja mwaka huu, itakayofanyika Makka, Saudia Arabia.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Taasisi bora za Hijja nchini (HAQI) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tanzania Charitable and Development Organizatia (TCDO), Swed Twalib wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ibada hiyo.

Alisema tayari baadhi ya Taasisi za Kiislamu nchini, zinaendelea na maandalizi mbalimbali ya kusimamia na kuratibu ibada hiyo ili kuhakikisha mahujaji watakaokwenda kwenye ibada hiyo, hawapati usumbufu kwa wakati wote watakaokuwa katika ibada hiyo.

Aliongeza kuwa mahujaji watakaokwenda katika ibada hiyo mwaka huu, wasiwe na wasiwasi kuhusu vyakula vya Kitanzania, kwani taasisi hizo zimejipanga kuweka vyakula vya nyumbani vilivyozoeleka ili kulinda afya za mahujaji zisitetereke na kushindwa kushiriki kikamilifu katika ibada hiyo.

“Mara nyingi katika miji ya Makkah na Madina kunakuwa na vyakula ambavyo sio rafiki kwa Watanzania, kwa kuliona hilo tumeona ni vyema tukaandaa chakula cha Kitanzania ambacho kitakuwepo wakati wote wa ibada,” alisema.