Mahiga ataka vijana kuwa wabunifu

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga amewataka vijana kujitahidi kuongeza nyenzo na mbinu, hasa katika ufundi na ubunifu ili waweze kujiajiri na kufanya vizuri katika fursa mbalimbali, zikiwemo biashara katika soko la pamoja kwenye mtangamano wa Afrika Mashariki.

Aliyasema hayo juzi jijini Dar es salaam, wakati akizindua kampeni ya Chungulia Fursa ‘Boda to Boda’ katika kongamano lililokuwa likizungumzia fursa zilizopo Afrika Mashariki, hasa kwa vijana ambao mara nyingi wamekuwa wakisahaulika katika mkondo wa biashara.

“Vijana mnapaswa kuongeza juhudi katika ubunifu na ukishapata ufundi wako unakuwa umepata kitu cha thamani kwa kuwa hakuna atakaye kunyang’anya hadi utakapokufa, hivyo pamoja na shahada zenu lakini mjifunze utaalamu ambao utawapa ajira au utawawezesha kujiajiri wenyewe,” alisema.

Alisema nchi zilizoendelea zilijua siri ya maendeleo ni biashara na ndilo chimbuko la utajiri, hivyo ushirikiano wa Afrika Mashariki katika masuala mbalimbali ikiwemo biashara utasaidia kuchochea maendeleo.