Mjane wa watoto kumi ateswa na wifi ‘mahakamani’

MJANE mwenye watoto 10, Sona Fumbi mkazi wa Chamwino mkoani Dodoma ametaka mahakama kuangalia haki za wajane wanaotaka kudhulumiwa mali zao ili wasiteseke kufuatilia kesi muda mrefu mahakamani.

Alisema hayo juzi wakati akitoa ushuhuda kwenye mkutano wa kutoa azimio la wanawake wa Tanzania juu ya haki za ardhi uliofanyika Kijiji cha Mloda Wilaya ya Chamwino. Alisema aliolewa mwaka 1978 na Abiseli Fumbi ambaye kwa sasa ni marehemu katika kipindi cha ndoa na mumewe walibahatika kupata watoto 10. Hata hivyo, alisema mumewe alipata saratani ya mguu ambapo alitumia muda mwingi kumuuguza hadi alipofariki mwaka 2009.

Alisema mwaka 2010 dada wa mumewe Eunice Fumbi alianza kumsimanga na kumtaka atoe nyumba na mashamba yote, ndipo alipokwenda baraza la kata kumfungulia kesi ambapo alishinda kesi hiyo. “Baada ya wifi kuona nimeshinda kesi akakataa rufaa mahakama ya wilaya akaweka wakili anayefahamika kwa jina la Kuwayawaya Kuwayawaya lakini tarehe za kesi wote walikuwa hawafiki mahakamani,” alieleza.

Alisema ilipofika mwaka 2015 alishinda kesi kutokana na mdai wala wakili wake kutofika mahakamani. “Wifi akakata tena rufaa akasema atasimamia kesi mwenyewe lakini mwaka huu 2017 nikashinda tena kesi na mahakama ikatoa amri ya mimi kulipwa gharama zote za kesi akakataa tena rufaa,” alisema.

Alisema sasa amekwenda mahakamani zaidi ya mara tatu Juni 29, Julai 3 na Julai 10 lakini mdai bado hafiki mahakamani. “Serikali inisaidie katika hili sasa sifanyi shughuli zangu kila mara niko mahakamani kwenye kesi, nawaza tu mahakamani, ninalazimika kufanya vibarua ili nipate nauli ya kwenda mahakamani kwenye kesi wakati wifi yupo na hafiki mahakamani na hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake,” alieleza.