RC ahimiza mfumo stakabadhi ghalani

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge amewaagiza viongozi wa Serikali ya Wilaya ya Namtumbo kuhakikisha hakuna zao linalouzwa holela badala yake kuwahimiza na kusimamia wakulima wauze mazao yao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani uliopendekezwa na serikali.

Dk Mahenge alisema mfumo huo umeonesha mafanikio makubwa katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Wilaya ya Tunduru ambayo wakulima wa zao la korosho wamenufaika sana baada ya kuuza zao hilo kwa mfumo huo.

Alitoa agizo hilo juzi hapa wakati akifungua rasmi soko la zao la tumbaku kwa msimu wa mwaka 2017 katika Mtaa wa Rwinga, Kata ya Rwinga wilayani Namtumbo. Kwa mujibu wake, kuanzia sasa hakuna zao litakalouzwa holela mkoani Ruvuma, kwani wanunuzi wanatumia nafasi hiyo kuwaibia wakulima na matokeo yake kusababisha wakulima kukataa tamaa baada ya kuona hakuna manufaa ya kuendelea na uzalishaji mashambani.

Dk Mahenge alisema kufunguliwa kwa soko la tumbaku mkoani Ruvuma ni ishara kuwa serikali ya awamu ya tano inawajali sana wakulima kwani serikali ndiyo iliyotafuta mnunuzi wa zao hilo Kampuni ya Premium kutoka Morogoro ambayo imeingia mkataba wa miaka saba na Sonamcu kununua tumbaku itakayolimwa mkoani Ruvuma.