Wadai kudhalilishwa kijinsia

“Hawa mgambo walifanya makosa kuwanyanyasa akinamama hawa hata kama walikuwa na makosa taratibu za wanaokiuka sheria si zipo; kwanini wadai ngono pia walikuwa hawafanyi biashara kwenye eneo lililokatazwa hivyo tutawatafuta na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua.”

Mwenyekiti wa Mtaa wa Maili Moja mjini Kibaha, Athuman Mkongota alisema hayo katika mkutano wa mtaa hivi karibuni aliposema, baadhi ya akinamama walilalamika ofisini kwake kuwa walitakiwa watoe rushwa ili wasitozwe faini kwa kudaiwa kufanya biashara kwenye maeneo yaliyokatazwa.

Alisema kitendo kilichofanywa na baadhi ya askari wa mgambo kwa kuwadai akina mama hao wafanyabiashara ndogo rushwa ya ngono, ni udhalilishaji usioweza kufumbiwa macho. Mwanahamisi Shomary, mmoja wa wauzaji wa samaki alisema tangu waondolewe kwenye eneo la stendi na kuhamia kwenye barabara za mitaa, wamekuwa wakisumbuliwa na mgambo hao.