Japan yajitosa tena kumaliza foleni Dar

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa zamani wa Japan na Mbunge mwakilishi wa wabunge wa Japan wanaoshughulikia masuala ya Afrika katika Bunge la nchi hiyo, Ichiro Aisawa amesema ameona tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam na atazungumza na serikali yake kusaidia kulitatua.

Aisawa alisema hayo jana alipofanya mazungumzo na Rais John Magufuli, Ikulu, Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida. Aidha, Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Japan kwa namna inavyoshiriki katika miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo miundombinu nchini na ameiomba isaidie kujenga barabara za juu au za chini makao makuu ya nchi, Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa katika mazungumzo hayo, Aisawa ametembelea miradi inayojengwa nchini na kampuni za Japan ikiwemo ujenzi wa barabara za juu (Flyover) wa Tazara na wa kuzalishaji umeme kwa gesi wa Kinyerezi.

Aisawa baada ya kutembelea miradi hiyo, alimhakikishia Rais Magufuli kuwa kampuni hizo zitafanya kazi nzuri na zitakamilisha kazi kama ilivyopangwa. Katika ziara hiyo, alijionea changamoto ya foleni za barabarani katika Jiji la Dar es Salaam.

Kuhusu msongamano huo, Aisawa alisema baada ya kuona changamoto hiyo ya foleni katika Jiji la Dar es Salaam, amebaini kuwa nchi yake inahitaji kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha miundombinu ya jiji hilo na aliahidi kufikisha ujumbe huo kwa Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe ili kuona namna ya kukabiliana nalo.

Aidha, Aisawa alimpongeza Rais Magufuli kwa uongozi mzuri, kupambana na rushwa na msukumo mkubwa anaoutoa katika maendeleo, juhudi ambazo zinasaidia kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za kijamii.

Kwa upande wake, Rais Magufuli pamoja na kumshukuru Aisawa kwa kuja Tanzania na alimhakikishia kuwa Tanzania inatambua mchango mkubwa ambao Japan inautoa katika maendeleo, na itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Japan katika masuala mbalimbali.

Dk Magufuli aliahidi kuwa serikali itahakikisha uwekezaji wa kampuni za Japan nchini unalindwa kama itakavyofanya kwa kampuni ya kutengeneza rangi ya Kansai Plascon ambayo awali ilijulikana kama Sadolin na kampuni inayozalisha betri za Panasonic nchini, ili uwekezaji huo ulete manufaa nchini.

“Naomba unifikishie ujumbe kwa Waziri Mkuu, Shinzo Abe kuwa Tanzania inamshukuru kwa ushirikiano huu mkubwa, tunamkaribisha sana Tanzania na kwa kuwa serikali yetu imehamia Dodoma tutafurahi sana kama Japan itaweka alamu ya urafiki wetu kwa kutujengea barabara za Dodoma mjini, iwe ni flyover au kilometa 20 za barabara, sawa tu,” Rais Magufuli alimweleza Aisawa.

Aidha, aliishukuru Japan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi jijini Dar es Salaam ikiwemo upanuzi wa barabara ya Mwenge – Morocco utakaoiwezesha barabara hiyo kuwa na zaidi ya njia nane, ujenzi wa barabara ya Tazara, ujenzi wa daraja la Gerezani njia nne, na barabara ya Bendera Tatu hadi Kamata.

Alimuomba mbunge huyo kwa kuwa ni mmoja wa wabunge wa Japan wanaoshughulikia masuala ya Afrika, kuwahamasisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Japan kuja kuwekeza zaidi nchini.