‘Deni la taifa ni mzigo kwa serikali’

MZIGO mkubwa kwa serikali kuhudumia deni la taifa, unaipunguzia uwezo wa fedha za kushughulikia upatikanaji wa huduma bora za jamii na maendeleo, imeelezwa.

Aidha, misamaha ya kodi inaikosesha serikali vyanzo vya mapato ya ndani ambayo yangesaidia kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo hivyo kuathiri maendeleo.

Hayo yamebainishwa kwenye ripoti ya Uwajibikaji wa Serikali kuu iliyofanywa na Taasisi ya Uwajibikaji wa Umma-WAJIBU kwa kushirikiana na taasisi ya utekelezaji ya ushirikiano wa Ujerumani na Tanzania (GIZ) kupitia mradi wa Utawala bora na Fedha za Umma.

Ripoti hiyo ni miongoni mwa ripoti tatu za uwajibikaji kwa serikali za mitaa, serikali kuu na mashirika ya umma zinazotokana na mapendekezo ya ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2015/16 zilizowasilishwa bungeni Aprili 13 mwaka huu.

Akizungumza kabla ya uzinduzi wa ripoti hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa WAJIBU, Ludovick Utouh, alisema ingawa ukubwa wa deni la taifa bado upo kwenye uwiano unaokubalika kwa kutumia vigezo vya Benki ya Dunia, ukubwa huo unaipunguzia uwezo serikali wa mapato ya kuleta maendeleo.

“Ukubwa wa teni la taifa unapunguza uwezo wa kupeleka huduma za kijamii kama vile afya, maji pamoja na kutekeleza miradi ya maeneleo, kwani serikali inapokusanya mapato, kipaumbele cha kwanza ni kulipa deni la taifa, hivyo kubaki na fedha kidogo,” alisema.