Lukuvi akemea mchezo mchafu viongozi wa vijiji

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewataka viongozi wa vijiji na vitongoji, kutogawa vijiji vilivyoingia katika mpango wa matumizi ya ardhi kwa kuwa wanaharibu mpango huo na kulazimisha kupimwa kwa mipaka ya vijiji.

Amesema kuwa viongozi hao wamekuwa wakigawanya vijiji kwa sababu za kisasa kwa lengo la kuongeza wapigakura, hali inayoharibu mpango huo. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ugawaji hatimiliki za kimila katika kijiji cha Nyange wilayani Kilombero, Morogoro jana, Lukuvi alisema serikali inatumia fedha nyingi kutekeleza Mradi wa Uwezeshaji Umilikishaji Ardhi (LTSP) katika kupima, kupanga na kugawa hatimiliki za kimila kwa wananchi.

“Wapo viongozi wa vijiji na vitongoji kutaka baadhi ya vijiji kugawanywa ili waongeze wapigakura au wanapoona wanakataliwa na wananchi, hivyo serikali hairuhusu vijiji vigawanywe kwa sababu za kisiasa hususani wakati wa uchaguzi kwani mpango huu tunatumia fedha nyingi,” alisema Lukuvi.

Alisema viongozi wanataka kugawa vijiji kwa ajili ya kutaka madaraka kwa sababu mwakani unaanza uchaguzi wa vijiji na vitongoji, hatua ambayo haitakubalika. “Maeneo yote ambayo yalishatayarishiwa mpango wa matumizi ya ardhi na kupewa hati za vijiji yasigawanywe.

Najua baadhi ya viongozi wamekaa na kutathmini kwamba baadhi ya vitongoji watakosa kura hivyo wagawe, hatukubali na hatutafanya..huu ni mchezo wa kisiasa,” alisisitiza.

Alieleza kuwa madiwani wakati wa uchaguzi, pia wanaadhimia kugawa vijiji bila kujali gharama zilizotumika katika mradi huo, mpango wa maendeleo wa Kata hiyo vijiji ikiwemo shule na baadaye wanachukiana huku serikali ikiingia gharama.

Aidha, alisema halmashauri za wilaya zinatakiwa kuainisha vijiji vyenye tabia ya kimji na kupeleka mapendekezo wizarani na kwamba azimio hilo linapaswa litimie ili mwisho wa mwaka huu atangaze Kidatu kuwa eneo la mipango ili wananchi wapangiwe maeneo yao na nyumba ziwe na hadhi na hati za kumiliki.

Alisema hadi kukamilika kwa mradi huo, kunalenga kubainisha maeneo yaliyopimwa, hatimiliki za kimila na maeneo yaliyopewa hadhi ya kimji ndani ya vijiji ili yaweze kupangwa kwa mujibu wa mipango miji.

Kwa mujibu wa Lukuvi, serikali imeshiriki lakini fedha nyingi zimetoka kwa wadau wa maendeleo ambao ni Denmark, Sweden na Uingereza, lengo mafanikio ya majaribio hayo yatakayopatikana yaweze kuenea katika wilaya nyingine za Tanzania.

“Tunawaomba msikwamishe mradi huo wa maendeleo badala yake msaidie ufanikiwe zaidi ya malengo ili mradi huo uweze kuenea na maeneo mengine,” alisema. Kwa upande wake, Mratibu wa LTSP, Godfrey Machabe alisema kuwa mradi huo unatekelezwa katika Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi na kwamba vijiji 160 vitanufaika na mradi huo ambapo 80 kutoka (Kilombero), 46 (Ulanga) na 32 (Malinyi).

Naye Balozi wa Denmark, Hebogard Jensen alisema wataendelea kuwa wametoa Dola za Marekani milioni 15.2 kwa ajili ya kufadhiri mradi huo. Alisema wataendelea kuisaidia Tanzania katika nyanja mbalimbali kwa ajili ya maendeleo yake.