Waliopokwa viwanda washindwa kujitetea

WAJUMBE zaidi ya 22 kutoka kwenye viwanda 10 vilivyopokonywa na serikali hivi karibuni kutokana na wawekezaji waliobinafsishiwa kuvitelekeza wameshindwa kujitetea mbele ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Msajili wa Hazina katika kikao kilichofanyika Dar es Salaam jana na hivyo serikali kusisitiza kutekeleza uamuzi wake huo kwa masharti makali.

Miongoni mwa masharti yatakayotumika wakati wa makabidhiano ya viwanda hivyo baina ya serikali na wawekezaji hao ni kutumika kwa rejista inayoonesha mali zilizokuwepo wakati kiwanda kinabinafsishwa ili kujiridhisha kama vitu vyote vipo kabla ya kukichukua.

Katika kikao cha jana, Serikali kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhelm Meru iliwataka wamiliki wa viwanda walioshindwa kuviendeleza kuwa inatosha na kuwataka kuvikabidhi haraka mikononi mwa serikali baada ya kukutana na wamiliki hao.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Msajili wa Hazina, Dk Oswald Mashindano kupitia vyombo vya habari juzi, viwanda vilivyoitwa kwenye kikao hicho cha jana ni Mkata Saw Mills, Kiwanda cha Korosho Lindi, Kiwanda cha Taifa cha Chuma, Manawa Ginnery, Tembo Chipboard, Mang’ula Mechanical Machine Tools, Mgodi wa Pugu Kaolin, Dabaga Tea Factory, Kiwanda cha Polysacks na Kilimanjaro Textile Mills-Arusha.

Dk Meru alisema kuwa mwaka 1992 Serikali iliona kuwa haiwezi kuviendesha viwanda ilivyokuwa inavimiliki kutokana na viwanda hivyo kusuasua na vingine kushindwa kabisa kufanya kazi, hivyo iliamua kuvibinafsisha kwa sekta binafsi ili waviendeleze.

Alisema jumla ya viwanda 156 vilibinafsishwa kuanzia mwaka 1992 hadi 2007. Kati ya viwanda hivyo, viwanda 62 vinafanya kazi vizuri kikiwemo Kiwanda cha Bia (TBL), Kiwanda cha Sigara (TCC) na viwanda vya saruji kama vile Tanga Cement na vinginevyo.

Aliongeza kuwa viwanda vingine 28 bado vinasuasua, 56 vimefungwa ingawa kuna juhudi zinaendelea ya kuvifufua baadhi yake kama vile Kiwanda cha Bora, na viwanda vingine 10 vilibinafsishwa kwa kuuza mali mojamoja kama vile mashine ziliuzwa peke yake, jengo peke yake na baadaye mashamba.

“Mikataba ya ubinafsishaji wa viwanda hivyo ilikuwa na masharti mbalimbali likiwemo sharti la kuviendeleza, lakini baada ya ukaguzi wetu, tukaona hakuna kilichofanyika na kama kipo kilichofanyika basi ni kidogo sana, jambo hilo ni kinyume na lengo la Serikali la kuvibinafsisha viwanda hivyo ili viendelezwe katika uzalishaji, vitoe ajira kwa wananchi, serikali ipate mapato na wao wapate faida,”aliseam Dk Meru.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, kikao hicho cha jana kilikuwa kinatoa fursa kwanza ya kusikiliza maoni ya wamiliki hao wa viwanda lakini pia ilikuwa fursa kwao kukabidhi viwanda hivyo kwa Serikali. Alisema Serikali ni sikivu na ndiyo maana iliamua kuwaita ili kuwasikiliza.

Naye Msajili wa Hazina, Dk Oswald Mashindano aliwaambia wamiliki hao wa viwanda walioshindwa kuviendeleza kuwa Serikali itatumia rejista inayoonesha mali zilizokuwepo wakati kiwanda kinabinafsishwa ili kujiridhisha kama vitu vyote vipo kabla ya kukichukua.

Hoja hiyo ya Msajili wa Hazina iliwafanya baadhi ya wajumbe kutaka ufafanuzi endapo umiliki wa kiwanda ulishahamishiwa kwa mtu mwingine kisheria. Akijibu hoja, Dk Mashindano alisema kuwa mkataba uliingiwa kati ya Serikali na mwekezaji wakati wa ubinafsishaji, hivyo kama mwekezaji alibadilisha umiliki wa kiwanda bila serikali kujua, hilo halitazingatiwa bali kitakachoangaliwa ni mkataba wa awali.

“ Kwa mfano kumbukumbu zinaonesha kuwa makubaliano ya ubinafsishaji yalikuwa kati ya Serikali na mwekezaji John, lakini makubaliano ya kuuziana kiwanda hicho kati ya John na mwekezaji B Serikali haiyajui, na kama ni hivyo, utaratibu ungefuatwa ili marekebisho ya umiliki kutoka mwekezaji wa kwanza kwenda mwekezaji wa pili yafanyike,” alieleza Dk Mashindano.

Wajumbe wapatao 22 kutoka viwanda hivyo waliitikia wito wa serikali wa kufika kweye kikao hicho jana. Ikumbukwe kwamba Agosti 11 mwaka huu, vyombo vya habari vilimnukuu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage akitangaza kuvifutia umiliki viwanda hivyo 10i kutokana na kushindwa kuzalisha au kuendelezwa.